Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa akizungumza na wananchi na wachimbaji wadogo wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo cha kuuza madini Januari 28, 2026.
...................................
Na Mwandishi Wetu, Kilindi
IMEELEZWA kuwa kwa Mtu yeyote kujihusisha na biashara ya kuuza na kununua Madini kinyemelea ni kosa la Uhujumu Uchumi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa amewataka wachimbaji wadogo kutumia Kituo cha Seuta ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya uendeshaji shughulu hiyo.
Mgandilwa alisema juzi kuwa, mtu yeyote atakayebainika kufanya biashara kinyemela ya ununuzi na utoroshaji wa madini atahusishwa na kosa la uhujumu Uchumi.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akizindua Kituo cha kuuzia madini kilichopo eneo la Seita kata ya Kikunde katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ambapo alipata fursa ya kuzungumza na Wamiliki leseni na wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya dhahabu wa eneo hilo.
Alisema,uanzishwaji wa kituo hicho lengo lake ni kuziba mianya ya utoroshaji madini hayo na hivyo kuiwezesha Serikali na halmashauri kuongeza mapato.
"Baada ya uzinduzi wa kituo hiki tutaanza operesheni kuwanasa wanaofanya biashara kinyemela,niwaombe kutumia kituo hiki"alisema Mkuu huyo wa Wilaya huku akiongeza kusema kuwa.
" Sheria ziko wazi kununua madini kinyemela ni kinyume na utaratibu ukikamatwa, ni kesi ya uhujumu uchumi na mzigo ulionao unapaswa kutakiwa kutaifishwa".
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya alisema, mpango uliopo ni kujengwa kwa Soko la madini litakalokuwa la kisasa litakalotoa fursa kwa wanunuzi wengi kukaa ili kuweza kuendesha shughuli zao.
Hatua hiyo itawasaidia Wadau kuendesha biashara ya madini kisasa sanjari na kuweka ushindani wa bei ya bidhaa husika, baada ya mazingira kuruhusu uwepo wa wanunuzi wengi kwa eneo moja.
Amewasihi Wadau wa sekta ya madini wenye nia ya kuhakikisha ujenzi wa Soko lililodhamiriwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kufanikisha ujenzi huo.
Faraja Mhelo ni mdau wa madini kupitia Wamiliki wa leseni za wachapakazi Group Abeid Kaisi na Ibrahim Kuwasa, alisema kuwa, kituo hicho ni fursa kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao awali walikosa Soko lenya uhakika kuendeshea shughuli zao.
Daniel Sembela ambaye ni Diwani wa Kata ya Kikunde, amewataka wachimbaji wa madini kuacha kuendesha shughuli zao kinyemela akiwasisitiza kutumia kituo husika.
Awali Kamishna wa Madini Mkoa wa Tanga, Naiman Samana alisema, kituo cha kuuzia madini cha Seita, kitarahisisha ununuzi wa madini kwa wachimbaji wadogo.
Aidha alisema, uwepo wa kituo hicho,kitaleta utatuzi wa changamoto ya ununuzi holela uliokuwa ukifanyika kwenye maeneo mbalimbali yasiyo rasmi.
Pamoja na hayo aliwasihi wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wilayani Kilindi kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa kwenye ununuzi na uuzaji wa madini katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya madini wilayani Kilindi,Samana alisema,ni kuongezeka kwa uzalishaji na uuzaji wa madini ya dhahabu, wilaya kujulikana Kimataifa na kuvutia wawekezaji wa kigeni.
Kwa kipindi cha 2024/2025 madini ya dhahabu yaliyozalishwa na kuuzwa wilayani Kilindi ni takribani Kilogram 57.7 yenye thamani ya Tsh 13,270,619,964.00 kati ya hizo kilogram 38.62 zenye thamani ya Tsh 9,264,345,337.00 zilizouzwa benki kuu ya Tanzania (B.O.T) na kulipwa mrabaha asilimia nne shilingi 370,573,813,48.00.
Kilogram 19.08 zenye thamani ya Tsh 4,006,274,627.00 ziliuzwa kwenye masoko mengine na kulipiwa mrabaha asilimia 6 Tsh 240,376,477.62 na ada ya ukaguzi Tsh 40,062,746,.27 na ushuru wa huduma uliokusanywa kutokana na mauzo hayo ni Tsh 33,176,549.91.
Diwani wa Kata ya Kikunde Daniel Sembela, akichaangia jambo kwenye uzinduzi huo.
Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Tanga Naiman Samana akizungumza.
Wadau sekta ya Madini wakiwa katika mkutano na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa wakati wa uzinduzi kituo cha kuuzia madini Seita
Uzinduzi ukiendelea








0 Comments