Watoto hujifunza heshima kwa kuona mfano wa watu wazima-hivyo kama tutasimamia ipasavyo mitandao inaweza kuwa daraja la mshikamano, si chimbuko la matusi.
................................................
Na Dotto Mwaibale
TANZANIA inakabiliwa na tabia mpya ambayo ni hatari kwa mshikamano wa taifa letu kwa kuibuka baadhi ya raia ambao hutumia mitandao ya kijamii kutukana, kudhalilisha na kushambulia viongozi wa nchi.
Tabia hii siyo tu ni kinyume cha sheria na maadili, bali pia ni tishio kubwa kwa ustawi wa maadili kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Nikiangazia madhara ndani ya familia zetu ni kwamba watoto na vijana wa kizazi hiki wanakua huku wakiangalia na kusikiliza matusi na kejeli kama jambo la kawaida, na taratibu huanza kuiga tabia hiyo.
Matokeo yake familia hupoteza nafasi ya kuwa mfano wa maadili na heshima. Migawanyiko ya kifikra na kiutamaduni huibuka, watoto huanza kudharau wazazi, ndugu na hata walimu. Hali hii huunda kizazi kisicho na misingi thabiti ya maadili.
Na ndani ya jamii mitandao ya matusi huzaa chuki na kejeli miongoni mwa majirani, wanavikundi wa kijamii, hata marafiki huanza kugombana kwa sababu ya uongozi na siasa.
Hii inaharibu mshikamano wa jamii, huunda misingi ya migongano ya kihisia, na kupunguza mshikamano wa kijamii.
Tukiruhusu vijana wakue katika mazingira haya huingia katika jamii wakiwa na hofu, chuki na dharau kwa wengine.
Tabia hizi chafu za kudhalilisha viongozi mitandaoni hutishia mshikamano wa taifa zima.
Tukumbuke viongozi wakubwa wanapodhalilishwa hadharani, heshima ya taifa huporomoka ndani na nje ya mipaka.
Na tusipokemea sasa madhara ya sumu hiyo endapo vijana watakosa mfano wa heshima, hugeuka na kuanza kudharau wazazi, taasisi muhimu za taifa kama shule, hospitali, mahakama na mifumo ya serikali.
Na tukifika huko hatimaye, mshikamano wa taifa hupungua na ndoto za maendeleo hubaki hewani.
Labda tukumbushane, kutukanana na kudhalilisha viongozi hakuharibu tu heshima ya mtu, bali huunda mazingira ya vurugu na migawanyiko, inayoweza kuathiri kizazi kizima cha taifa.
Badala ya kutoa lugha zisizofaa, ni vema; kuhimizana juu ya uwepo wa mazungumzo na maridhiano kati ya wananchi na serikali, hususan katika ushirikishwaji wa wananchi kwenye sera na maamuzi.
Baraka ya mapinduzi ya teknolojia kwa ujio wa mitandao itumike kwa hoja, elimu na mshikamano, siyo matusi.
Wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu watu wanaomtukana Rais mitandaoni.
Mhariri wa Chumba cha Habari Clouds Media, Joyce Shebe anasema “ Mimi siku zote si muumini wa kumshambulia matusi au kumvua mtu utu wake kama unahoja weka mezani tafuta njia sahihi za kuzifikisha.
Anasema watu wasitumie mitandao kuvuana nguo, tusitumie kudhalilishana au kukengeuka maadili yetu kwa sababu mitandao ni kitu rahisi ambacho kila mtu anaweza kutumia mahali popote.
Kwa hiyo mimi si muumini wa hulka au tabia hizo, Natamani kuona watu wenye hoja za msingi kama viongozi wetu wamekosea basi zitafutwe njia sahihi za kufikisha hoja , malalamiko hata tuhuma, Ndiyo maana kuna mahakama, polisi, Serikali za mitaa.
Anasema kuna mahala ambapo tunaweza kufika na kutoa malalamiko yetu, tuhuma zetu, mashitaka yetu lakini tusitwezane kwa sababu tu mitandao imekuwa kitu rahisi na kila mtu anaweza kuitumia.
“Binafsi kiukweli nafadhaika pale ambavyo naona mitandao ya kijamii inatumika vibaya kwasababu hata huyu ambaye anamtukana rais ageuze kama Rais ni Mama yake, Baba yake mzazi ni rahisi kiasi hicho kumtukana mtu aliyekuzidi umri na unaenda mbali zaidi ni kiongozi mkuu wan chi ni rahisi kiasi hicho kumtukana,” alihoji Shebe.
Aliongeza kuwa wakati mwingine tuangalie namna ambavyo tunatumia mitandao yetu kwa sababu sheria zipo hazijalala na sheria hainaga msamaha kwamba mimi nilikuwa sijui. Sheria ipo umekengeuka utatiwa nguvuni yenyewe inazungumza mwisho wa siku unaweza kujikuta unaingia kwenye mtanziko wa kisheria kwa sababu tu ya matumizi mabaya ya mitandao.
Alisema hiki kipindi ambacho tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu mambo yanakuwa ni mengi mitandao inatakiwa itumike kwa hekima, busara bila ya kusahau maadili yetu.
Aliongeza kuwa hata sisi ambao wengi wetu tupo kwenye kuamini katika dini tofautitofauti hama maandiko tofauti inasaidia tukirudi kwenye mstari wa imani zetu kwamba kuna mahala inakatazwa kutoa maneno ya namna hiyo mwisho wa siku tunapaswa kuilinda nchi yetu.
Shebe aliongeza kuwa anatamani kuona tukitumia mitandao yetu vizuri na kuvuka salama kwenye uchaguzi na kusisitiza kuwa kama kuna wtu wanahoja za msingi kuna vyombo vya sheria vimewekwa hivyo vitumike kuwasilishiwa malalamiko na mashitaka.
Kwa upande wake Peter Godfrey mkazi wa Sumbawanga wenyeji mkoani Rukwa anasema wanaomtukana rais wamekosa uzalendo na maadili na kueleza kuwa watanzania hatujalelewa katika hali hiyo iliyokosa heshima.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Maji Matitu’ A’ Jimbo la Chamazi Kata ya Mianzini, Hawa Omari anasema ana kerwa sana na wanaomtukana Rais Samia mitandaoni na kuwa jambo linalosikitisha zaidi wengi wanaofanya hivyo ni wanawake.
“Sisi wanawake badala ya kujivunia na kumpa heshima rais wetu ambaye ni kiongozi wa kwanza katika nchi yetu kuwa rais badala yake ndiyo tunamuandama kwa kumtukana jambo hilo halikubalika hata kidogo,” alisema.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Rukwa, God Mwanisawa alisema anashangaa kuona kila siku watu wakiibuka mitandaoni wakimtukana Rais na akapongeza kazi nzuri inayofanywa na jeshi la polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya kuwakamata watu hao wanaotoa matusi mitandaoni dhidi ya viongozi na makossa mengine ya kimtandao.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbinga, Angelo Madundo anasema mtu ambaye ni mzalendo hawezi kumtukana kiongozi wan chi na kuwa wanaofanya hivyo watakuwa na changamoto ya kisaikolojia.
Alisema Rais Samia alipoichukua nchi ameimarisha usalama na nchi imetulia hivyo wanapotokea watu wachache miongoni mwetu kuanza kumtukana kwa sababu zao ambazo hazieleweke wanapaswa kupuuzwa kwani nchi hawezi kuendeshwa kwa kusikiliza kelele zao.
Alisema nchi inaendeshwa kwa kufuata katiba na inalindwa na vyombo vya ulinzi na usalama hivyo kila mtanzania anawajibu wa kuilinda na si vinginevyo.
Uchaguzi si vita; ni sherehe ya kidemokrasia, uhuru wa maoni ni muhimu, lakini si leseni ya vurugu au matusi.
Kila mmoja ana wajibu wa kuilinda amani, heshima na mshikamano wa taifa kama msingi wa maendeleo.
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari alisema wamejipanga kuhakikisha watu wote wanaotumia mitandao kumtukana Rais wanakamatwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.
Uchaguzi sio vita ni sherehe ya kidemokrasia. Wananchi wakiwa kwenye moja ya mikutano ya kisiasa.
0 Comments