Mtendaji Mkuu wa Shirika la ESTL linalotekeleza PJT-MMMAM mkoani Singida, Joshua Ntandu akifafanua jambo kwenye kikao hicho kilichofanyika Septemba 22, 2025.
............................
Na Abby Nkungu, Singida
ZAIDI ya Sh milioni 668.3 zimetumika kutekeleza shughuli mbalimbali za lishe kwenye halmashauri saba za mkoa wa Singida katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Katibu Tawala wa mkoa wa Singida, Dk Fatuma Mganga alibainisha hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa Kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa - Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) kilichofanyika mjini hapa jana.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala, Boaz Kajigili, Dk Mganga alisema kuwa kiasi kilichotumika ni sawa na asilimia 89.58 ya jumla ya Sh milioni 746.03 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya afua hiyo.
"Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa kuwekeza katika Afya na lishe ya mama na mtoto kama msingi imara na mkakati mmojawapo wa kufanikisha maendeleo thabiti katika nchi, ndio maana imetoa kiasi hicho cha fedha. Ni dhahiri kuwa lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote" alifahamisha.
Alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha kilitumika kununua mahitaji ya kutengeneza maziwa dawa kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo, kuandaa mapishi darasa, uanzishwaji wa bustani shuleni, kuendesha vikao vya tathmini za Mkataba wa lishe, vikao vya kamati za lishe, ukaguzi wa vyakula masokoni na viwandani na usimamizi shirikishi wa huduma za lishe.
Alitanabahisha kuwa mkoa umejikita katika kuhamasisha ulaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kupambana na matatizo yatokanayo na upungufu wa madini ya vitamini ambapo jumla ya mashine 33 za kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi zimefungwa katika halmashauri na tayari shule 206 zinasaga unga kwa kutumia mashine hizo kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi.
"Ni rai yangu Programu Jumuishi ya Taifa - Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto itumike kama fursa ya kutekeleza suala la lishe kwa watoto katika maeneo yenu ili kuondokana na matatizo ya utapiamlo; hususan udumavu ili kujenga jamii yenye siha nzuri, uwezo wa kubuni na yenye tija kiutekelezaji" alisema Dk Mganga.
Aidha, aliwaasa Watendaji wa Serikali kuendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali waliopo kwenye Mamlaka zao ili kuhakikisha afua zote tano zilizopo kwenye Peogramu ya MMMAM zinatekelezwa ipasavyo hadi mkoa ufikie maono ya "Watoto wote wa Singida wapo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu".
Awali, Mtendaji Mkuu wa Shirika la ESTL linalotekeleza PJT - MMMAM mkoani Singida, Joshua Ntandu aliiomba Serikali ya mkoa kuangalia namna bora ya kupambana na tatizo la ukeketaji watoto wa kike mkoani humo kutokana na watekelezaji wa vitendo hivyo kuwa wabunifu zaidi kwa sasa kuliko ilivyokuwa hapo zamani katika kukwepa mkono wa Sheria.
Alisema kuwa japo takwimu za Taifa zinasema ukeketaji Singida ni asilimia 45 kwa watoto walio chini ya miaka mitano, ukweli ni kwamba si rahisi kupata takwimu sahihi za vitendo hivyo kwa sasa kutokana na namna vinavyofanyika kwa usiri mkubwa na katika umri ambao mtoto huwa hajitambui lakini hapo anapokuwa mkubwa na kubaini kukeketwa, huumia mno kiakili na kisaikolojia.
Baadhi ya washiriki wa kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa-Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa mmoja wa wasilishaji taarifa
0 Comments