........................................
Na Mwandishi Wetu, Babati
Kikundi cha wanawake cha SELF LOVE cha wilayani Babati, mkoani Manyara, kimeshiriki michezo ya kirafiki na timu ya wanawake ya Tanzanite ya wilaya hiyo, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi, hususan wanawake, kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Mgeni rasmi katika michezo hiyo, Ndg. Ismail Kashasha, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Babati Emanuela Kaganda, aliwapongeza wanawake hao kwa ushirikiano na ubunifu wao katika kutumia michezo kama chachu ya kuhamasisha ushiriki wa kisiasa.
Kashaha alitoa wito kwa wananchi wote wa wilaya hiyo kujitokeza kwa amani siku ya uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuchangia maendeleo ya wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Aidha, ameipongeza kampuni ya DUTCHKONA kwa mchango wake mkubwa katika jamii, ikiwemo kudhamini michezo hiyo na kusaidia ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Komoto wilayani humo.
Awali, akisoma risala kwa niaba ya waandaaji, Mratibu wa mashindano hayo Bi. Esther Chessa alisema lengo kuu la mashindano ni kuwaunganisha wanawake katika kushirikiana kijamii na kiuchumi, pamoja na kuhamasishana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mdhamini mkuu kutoka kampuni ya DUTCHKONA, kupitia vinywaji vyake vya Jogoo na Kisungura, Bi. Noreen Mollely, alisema kampuni yao imevutiwa na juhudi za wanawake wa SELF LOVE, na kuahidi kuendelea kuwashika mkono katika shughuli mbalimbali za kijamii na za maendeleo.
Michezo hiyo ilihudhuriwa na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Babati, ambapo pamoja na burudani, ilitumika kama jukwaa la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa amani na umoja.
0 Comments