Na WMJJWM – Iringa
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Utekelezaji wa Programu
ya Kizazi Chenye Usawa, Mhe. Angela Kairuki amepongeza juhudi kubwa
zinazofanywa na wanawake wa Mkoa wa Iringa kupitia Majukwaa ya Uwezeshaji
Wanawake Kiuchumi.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo tarehe 19, Juni 2025 mkoani Iringa wakati wa
ziara ya kufuatilia utekelezaji wa programu hiyo katika ngazi ya mkoa
pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto katika miradi ya uzalishaji.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Kairuki amesema amevutiwa na mshikamano,
ubunifu na jitihada za wanawake katika kuanzisha na kuendesha miradi ya
uzalishaji.
Ameongeze kuwa Kamati hiyo imefanya ziara mkoani humo kwa lengo la
kutembelea miradi mbalimbali ya wajasiriamali, vikundi vya wanawake,
vijana, na watu wenye ulemavu, pamoja na majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi.
Aidha, Mhe. Kairuki amewahimiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali kwani fursa hizo ni
nyenzo muhimu za kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Ni wakati wa kuhakikisha kuwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
mnachangamkia kikamilifu fursa zinazotolewa na serikali kuwawezesha
kiuchumi” amesema Mhe. Kairuki
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi Zanzibar
ambaye pia ni Mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Mgeni Hassan Juma amesema kuwa
ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usawa wa kijinsia
unatekelezwa kwa vitendo katika ngazi zote za jamii.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Juliana Kibonde,
amesema kuwa Wizara kupitia Idara hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu
na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha kuwa fursa
mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi zinazotolewa na Serikali zinawafikia na
kuwanufaisha kwa vitendo.
Kwa upande wa wanufaika kupitia Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa
wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kusimamia utekelezaji wa programu hiyo kwa
moyo wa dhati.
0 Comments