Subscribe Us

MAPATO YA HALMASHAURI YA WILAYA YA BABATI YAONGEZEKA MARA MBILI NA ZAIDI

Halmashauri ya Wilaya ya Babati imefanikiwa kuongeza mapato yake ya ndani kutoka shilingi bilioni 1.6 hadi bilioni 3.9 katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Anna Mbogo, wakati wa kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani lililoanza kazi Januari 2020.

Bi. Mbogo amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa vyanzo vya mapato, matumizi ya mifumo ya kielektroniki, pamoja na ushirikiano mzuri kati ya wataalamu na viongozi wa kisiasa katika Halmashauri hiyo.

“Hii ni hatua kubwa sana kwetu kama Halmashauri Kuongeza mapato kutoka bilioni 1.6 hadi bilioni 3.9 si jambo dogo, na ni matokeo ya kazi ya pamoja, uadilifu na dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu,” alisema Bi. Mbogo.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri aliyemaliza muda wake, Mhe. John Noya, amewataka wataalamu wa Halmashauri kuendeleza juhudi hizo na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa mapato, kwa kuwa mapato ni “moyo wa Halmashauri”.

“Mapato haya yakisimamiwa vizuri, maana yake ni huduma bora zaidi kwa wananchi,kama viongozi wa kisiasa tumefungua njia, wataalamu sasa lazima waimarishe na kulinda mafanikio haya,” alisema Mhe. Noya.

Katika kipindi hicho cha miaka mitano, Halmashauri ya Wilaya ya Babati pia imepata hati safi kwa miaka yote mitano mfululizo kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jambo linalodhihirisha uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma.

Aidha, hoja za CAG zimepungua kwa kiwango kikubwa, kutoka zaidi ya 60 hadi kufikia chini ya tano, jambo ambalo limepongezwa na madiwani katika kikao hicho.


 

Post a Comment

0 Comments