JAMII ya wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara imehimizwa umuhimu wa kutumia maji safi na tiririka katika kusafisha jeraha la mtu aliyeng'atwa na mbwa mwenye ugonjwa wa Kichaa.
Wito huo umetolewa leo Septemba 26, 2025 na Daktari wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo, Dkt. Joseph Sijapenda, wakati akitoa elimu ya afya kuhusu Kichaa cha Mbwa kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiteto mkoani Manyara."Iwapo utang'atwa na mbwa hakikisha unasafisha jeraha kwa maji safi na tiririka na weka maji mengi kuzuia vimelea visisambae," amesema Dkt. Sijapenda.
Kwa upande wake Dkt. Joanne Maro kutoka Wizara ya Afya amekumbushia umuhimu wa matumizi ya namba 199 bila malipo katika dharura za afya ikiwa ni pamoja kutoa taarifa za kung'atwa na mbwa mwenye ugonjwa wa Kichaa.
"Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni timu moja katika kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa hivyo, nikumbushe pindi inapokumbwa na changamoto waweza kupiga simu 199 bila malipo kwa ushauri zaidi na wa haraka," amesema Dkt. Maro.
Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari Kiteto Bw. John Kimaro amesema elimu ya afya kuhusu magonjwa yaenezwayo kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ikiwemo kichaa cha mbwa ina umuhimu mkubwa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
"Wanafunzi ni muhimu sana kuzingatia elimu hii kuhusu kichaa cha mbwa na mchue tahadhari dhidi ya mbwa wanaozurura na msipuuze kwani unaweza kukutana na swali kuhusu kichaa cha mbwa kwenye mitihani, " amesisitiza Bw. Kimaro.
Nao baadhi ya Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Kiteto akiwemo Doria Kilave pamoja na Msafiri Silange wamevutiwa na elimu hiyo kwani wamejua mambo mengi ikiwemo umuhimu wa kuwahi vituo vya kutolea huduma za afya, matumizi ya 199 na umuhimu wa kuchanja mbwa.
0 Comments