Subscribe Us

MKUU WA WILAYA BABATI AKUTANA NA WANANCHI KUSIKILIZA KERO

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuella Kaganda, akizungumza na wananchi wakati akisikiliza kero mbalimbali. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Amosi Yohana.
......................................

Na Mwandishi Wetu, Manyara

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuella Kaganda, ameendelea na utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi kwa kutembelea Kata ya Magugu ambapo amekutana na wananchi, wazee na viongozi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara.

Katika mkutano huo, Mhe. Kaganda amewaonya wananchi wanaouza mali za familia, hususan ardhi, bila kushirikisha wenza wao wa ndoa, akisisitiza kuwa tabia hiyo isiyokubalika ni chanzo cha migogoro ya kifamilia. Amezielekeza Serikali za mitaa kutumia mamlaka walizopewa kwa haki, kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wote badala ya kuzua taharuki au kuegemea upande mmoja.

Aidha, amepokea kero mbalimbali na kutoa maelekezo kwa wataalamu kutoka idara husika kuhakikisha wanakwenda moja kwa moja katika maeneo yenye changamoto, hasa katika sekta ya nishati kupitia TANESCO na miundombinu ya barabara kupitia TARURA, ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Katika hatua nyingine, DC Kaganda amewaonya watumishi wa umma ambao hawatimizi wajibu wao ipasavyo, hasa katika vituo vya afya na zahanati, akiwataka wasimamizi wao kuwachukulia hatua stahiki mara moja.

Akihitimisha mkutano huo, ametoa rai kwa wananchi kuendeleza amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura na kuachana na dhana potofu kuhusu mchakato huo, akisisitiza kuwa msingi wa uongozi wake ni "Amani na Maendeleo."

Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Kero zikitlewa.


Kero zikitolewa kwa Mkuu wa Wilaya. 

Post a Comment

0 Comments