Na. OWM-KVAU
Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa
kutangaza nyongeza ya Kima cha chini cha Mshahara kwa sekta binafsikwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/= ambapo kitaanza
kutumika rasmi ifikapo 1 Januari, 2026 hatua inayolenga
kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua maslahi ya wafanyakazi nchini.
Akitangaza
amri hiyo, leo (17 Oktoba 2025) Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na
waandishi wa habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Ridhiwan Kikwete alisema mchakato wa upangaji wa Kima kipya cha chini cha mshahara umekamilika na
kwamba umezingatia mamlaka aliyopewa chini ya
Kifungu cha 39 (1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300.
“Kwa mujibu wa Amri hiyo, Sekta za Kima cha chini cha Mshahara zimeongezeka kutoka 13 za mwaka 2022 hadi 16 kwa mwaka
2025 na kutoka sekta ndogo 25 za mwaka 2022 hadi 46 kwa mwaka 2025. Kima cha
chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi
275,060/= hadi 358,322/= na kitaanza kutumika rasmi tarehe 1 Januari, 2026”, alisema Waziri
Ridhiwani Kikwete.
Kwa mujibu wa
Waziri Ridhiwani , Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara imegusa sekta za kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji,
hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi,
nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyinginezo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kima cha Chini
cha Mishahara kwa Sekta Binafsi Dkt. Suleiman Rashid Mohamed alisema mchakato
wa majadiliano ulikuwa shirikishi ambapo vyama vya wafanyakazi, waajili na
waajiliwa vilishiriki kikamilifu katika hatua zote.
Naye Naibu Katibu Mkuu Shirikishio la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Rehema Ludanga alisema kitendo cha Serikali kutangaza
amri ya kupanda kwa mishahara kwa kima cha chini cha sekta binafsi ni faraja kwa
wafanyakazi nchini kwani kimeonesha dhahili namna Serikali inavyothamini maslahi
ya wafanyakazi nchini.
Rehema aliongeza kusema ni wakati sasa waajili wote
katika sekta binafsi kutekeleza amri hiyo kwa kupandisha mishaharana ikibidi zaidi ya kiwango kilichotangazwa ili
kuongeza maslahi bora ya wafanyakazi wao .
Suzanne Ndomba-Doran Afisa Mtendaji Mkuu Chama cha
Waajili Tanzania (ATE) akizungumza kwenye kikao hicho alisema Chama kilishiriki
kikamilifu kwenye mchakato kupitia kamati ya wataalam ambapo maoni yote yaliyokusanywa
toka mikoa yote nchini na yamefanyiwa kazi hatua inayotoa urahisi wa
utekelezaji wa amri hiyo..
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo aliwasihi waajili kutumia muda huu kabla ya kufika tarehe 01 Januari 2026 kufanya mazungumzo yatakayopelekea kubadilisha ulipaji wa mishahara kwa mujibu wa amri iliyotangazwa na Serikali na kwamba ATE itaendelea kutoa elimu na taarifa kwa waajili wote nchini kutekeleza amri hii.
0 Comments