Subscribe Us

SERIKALI YAZIDI KUSOGEZA HUDUMA ZA ARDHI KWA WANANCHI NZEGA

Na Mwandishi Wetu – Nzega 

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kupitia Kliniki za Ardhi.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2025 Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, Tumaini Gwakisa amesema: “kliniki hii itahudumia wananchi kutoka kata mbili kati ya tano ambazo ni Nzega Mji Magharibi yenye mitaa minne na Nzega Mji Mashariki yenye mitaa sita na wananchi kutoka kata nyingine wakifika watapata huduma pia.”

Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, zaidi ya wananchi 818 watanufaika na huduma zitakazotolewa kupitia kliniki ya ardhi.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze amesema kuwa katika kliniki hiyo wananchi wote watakaofika watapewa elimu ya namna ya kufungua akaunti katika mfumo wa E-Ardhi utaowawezesha kufanya maombi mbalimbali ya masuala ya ardhi.

‘‘Huduma zinazotolewa ni Utoaji wa hati miliki za ardhi papo kwa papo, Utatuzi wa migogoro ya ardhi, Makadirio ya kodi ya pango la ardhi, Uhuishaji milki zilizoisha muda wake pamoja na kutoa Elimu na ushauri kuhusu masuala ya ardhi.”

Naye mkazi wa Nzega, Gabrian Joseph ameshukuru jitihada za Serikali kuwafikishia wananchi huduma kupitia kliniki za ardhi kwa kuwa zimewapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo na kuomba nguvu hii iendelee kote nchini.

Kliniki hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha usimamizi bora wa ardhi nchini.

Post a Comment

0 Comments