Mgombea ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, amesema lengo kuu la Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora kwa kupata huduma zote muhimu za kijamii, kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Magara, Sillo alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha dhamira thabiti ya kuendelea kusogeza huduma za maendeleo kwa wananchi vijijini.
“Kupitia Ilani mpya ya CCM, miradi ya maji, afya, elimu, barabara na umeme itaendelea kupelekwa kwa wananchi wote. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma kimaendeleo,” alisema Sillo.
Ameongeza kuwa changamoto zilizopo katika kata ya Magara, zikiwemo barabara zisizopitika na upungufu wa miundombinu ya kijamii, zitafanyiwa kazi mara baada ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Mzee Dodo Duguli, aliyewahi kuwa Katibu mwenezi wa kwanza wa CCM Mkoa wa Manyara, amesema chama hicho kimeendelea kuwa nguzo ya amani, umoja na upendo nchini kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
“CCM imejenga misingi ya amani na upendo. Ndiyo maana leo tunashuhudia uchaguzi unakaribia kufanyika kwa utulivu na ushiriki wa wananchi wote,” alisema Duguli.
Naye Mgombea udiwani wa kata ya Magara, Gonzalez Mkoma, amewataka wananchi kuendelea kuiamini CCM, akibainisha kuwa mahitaji yao makubwa ni barabara za uhakika, kidato cha tano na sita, kituo cha afya, mradi wa umwagiliaji, umeme, maji safi na shule ya msingi katika kijiji cha Maweni.
“Wananchi wa Maweni wanatembea zaidi ya kilomita 15 kufuata shule, jambo hili lazima tulimalize. Tuna imani kubwa kuwa CCM itapata kura asilimia 99.9 hapa Magara yenye wapiga kura zaidi ya elfu kumi,” alisema Mkoma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati Vijijini, Jackson Haibey, amesema chama hicho kinaendelea kufanya kampeni kwa amani huku kikiweka msisitizo kwa wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, ili kuchagua viongozi watakaoendeleza maendeleo nchini.
0 Comments