Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa watendaji kutoka Kituo cha Nishati cha Oman uliofika, Ikulu kuelezea hatua za miradi wanayoisimamia Zanzibar ukiwemo miradi ya Maji, Nishati na ukarabati wa Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia.
.......................................
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, amesema miradi ya kimkakati inayoendeshwa Zanzibar inahitaji kuzingatia
wakati katika utekelezaji wake ili kuleta tija kwa Taifa
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na Ujumbe wa
watendaji kutoka Kituo cha Nishati cha Oman uliofika kuelezea hatua za miradi
wanayoisimamia hapa Zanzibar ukiwemo miradi ya Maji, Nishati na ukarabati wa
Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia.
Rais Dk. Mwinyi ameuhakikishia ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itawapa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha miradi hiyo
aliyoielezea kuwa na umuhimu mkubwa kwa Uchumi wa Zanzibar, maendeleo na ustawi
wa wananchi wake.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho, Abdallah Humaid Al Ma’amary alisema, moja ya maboresho ya Mji Mkongwe ni kuufanya kuwa mji wa kisasa (Smart City) bila kuharibu uhalisia wa mji huo na kuzingatia vigezo na miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwa ni urithi wa dunia na kielelezo muhimu cha historia ya Zanzibar.
0 Comments