Subscribe Us

RC SINGIDA: NITAWASHANGAA NITAKAPOSIKIA MMEENDA KUIBOMOA NCHI

Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Mhe. Halima Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi akihutubia kwenye mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida yaliyofanyika Desemba 2, 2025.

................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amewaambia Wahitimu wa masomo wa mwaka 2024/ 2025 wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida  kwa jinsi walivyoandaliwa vizuri na Taasisi hiyo kuitumikia nchi atawashangaa iwapo watashiriki maandamano yanayotajwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yatafanyika Desemba 9, 2025.

Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo wakati akihutubia katika mahafali ya 23 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Desemba 2, 2025 mkoani humo.

“Serikali kupitia TIA Kampasi ya Singida imefanya kazi kubwa ya kuwaandaeni kwa ajili ya kulitumikia taifa hivyo nitashangaa kusikia eti na ninyi mtaenda kushiriki kuibomoa nchi yetu,” alisema Dendego.

Alisemma Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ili kutoa elimu katika mazingira bora ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi.

“ Leo ni siku ya furaha lakini pia ni mwanzo wa safari mpya katika maisha yenu. Elimu mliyoipata ni nguzo muhimu ya mafanikio, lakini dunia ya saasa inahitaji maarifa yanayoenda sambamba na teknolojia,” alisema Dendego.

Alisema katika zama hizi za mapinduzi ya kidijitali na Akili Unde (AI) soko la ajira limebadilika kwa kasi. Ajira nyingi sasa zinahitaji ujuzi wa teknolojia, ubunifu, na uwezo wa kubadilika hivyo waikumbatie katika kazi zao ili kuongeza ufanisi, ubunifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.

Dendego aliwaaambia wahitimu hao kutumia mitandao ya kijamii kwa maendeleo kwa kujitangaza kibiashara, kujifunza na kuunda mtandao wa fursa (Networking) badala ya kuitumia vibaya.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo akizungumza kwenye mahafali hayo, alisema mwaka huu wa masomo TIA Kampasi ya Singida inajivunia kutoa jumla ya wahitimu 1,490 (wanawake 733 sawa na asilimia 49.2, na wanaume 757 sawa na asilimia 51.8)

Alisema Kati yao ngazi ya cheti cha awali ni wahitimu ni 388, Astashahada 389, shahada 373 na shahada 340.

Profesa Pallangyo alisema wahitimu hao wanawakilisha takribani asilimia 14.4 ya wahitimu wote 10,334 wa mwaka wa masomo 2024/2025 katika kampasi zote nane za TIA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael alisema Udahili katika Kampasi ya Singida umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na kuwa katika mwaka wa masomo 2024/ 2025 kampasi hiyo ilidahili jumla ya wanafunzi 2,623 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24, ikilinganishwa na wanafunzi 2,115 kwa mwaka 2021/ 2022 na kuwa hiyo inaonesha kuongezeka kwa imani ya elimu inayotolewa TIA. 

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo akizungumza wakati akitoa taarifa kwenye Mahafali ya 22 ya taasisi hiyo Kampasi ya Singida yaliyofanyika jana Desemba 2, 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael, akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Mhe. Halima Dendego, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo na Mkurugenzi Mkuu wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema wakiwa kwenye mahafali hayo.
Brass Band ikitoa burudani kwenye mahafali hayo.
Wahadhiri wa chuo hicho wakishiriki mahafali hayo.
Wanafunzi wakiwa katika maandamo kusherehekea kuhitimu kwao.
Wahitimu wakiserebuka kwenye mahafali hayo.
Wazazi na Walezi na ndugu, jamaa na marafiki wa wahitimu hao wakiwa kwenye mahafali hayo
Waandishi wa habari wakiwajibika katika kuchukua taarifa mbalimbali kwenye mahafali hayo.
Burudani ya ngoma ya asili ya kabila la Wanyaturu ikitolewa.
Wahitimu wakitunukiwa vyeti vyao.
Wahitimu wakiwa kwenye mahafali hayo.

Post a Comment

0 Comments