Subscribe Us

CCM MANYARA YAPONGEZWA KWA KUTEKELEZA ILANI

Toima awaomba wananchi waendelee kukiamini chama chao

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Peter Toima, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Hanang’, uliofanyika kata ya Gehandu Srptemba 17, 2025.

.......................................

Na Mwandishi Wetu, Hanang'

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara, Peter Toima, amesema kuwa miradi yote mikubwa ya kitaifa na kimkoa iliyoelezwa kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 imetekelezwa kwa mafanikio makubwa, hivyo chama hicho kinastahili pongezi na kupewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Hanang’, uliofanyika kata ya Gehandu, Toima amesema utekelezaji huo umedhihirisha uimara wa CCM na nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Uzinduzi huo uliongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Namelok Sokoine, huku mgombea ubunge wa jimbo hilo akiwa ni Asia Halamga.

"Tofauti ya CCM na vyama vingine ni kwamba sisi hatuahidi tu, bali tunatekeleza. Katika kipindi cha miaka minne, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza nchi kwa ufanisi mkubwa, amedhihirisha kuwa ni kiongozi mwenye maono makubwa, mnyenyekevu, mchapakazi, na mwenye utu. Ni mfano wa kuigwa na hata mataifa mengine,” alisema Toima.

Aidha, amewaomba wananchi wa mkoa wa Manyara kuhakikisha wanampigia kura nyingi za ndiyo Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nafasi ya urais, pamoja na wabunge na madiwani wote wa CCM kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Akitoa takwimu za wanachama na wapiga kura, Toima amebainisha kuwa mkoa wa Manyara una jumla ya wakazi milioni 1,892,000, ambapo kati ya hao waliandikishwa kupiga kura ni milioni 1,105,000.

“Kwa idadi hii kubwa ya wapiga kura, naamini wananchi wa Manyara watatoa kura za kishindo kwa CCM ili kuhakikisha maendeleo yanaendelezwa,” aliongeza Toima.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara, Peter Toima, akiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Namelok Sokoine kwenye uzinduzi huo. 

Post a Comment

0 Comments