Mgombea Udiwani Kata Kiru Babati, mkoani Manyara ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari ya Kiru, Joseph Siima Sanka (katikati) akikabidhi cheti.
...................................
Na Mwandishi Wetu, Babati
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiru, Isack Makena, amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, shule hiyo imepata mafanikio makubwa katika taaluma na miundombinu, ikiwemo kutokuwapo kwa mwanafunzi yeyote aliyepata 'division' ziro kwa miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza wakati wa mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo, Makena amesema kuwa juhudi za walimu, wanafunzi na wazazi zimekuwa nguzo kuu ya mafanikio hayo, huku akibainisha kuwa shule hiyo pia imefanikiwa kujenga madarasa mapya matano (5) yaliyokamilika kati ya mwaka 2021 hadi 2024 kwa ufadhili wa Serikali.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika elimu. Ujenzi wa madarasa haya umetusaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza ufanisi katika kujifunza,” alisema Mwalimu Makena.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi, Joseph Siima Sanka mgombea udiwani CCM Kata ya Kiru ameipongeza menejimenti ya shule na walimu wote kwa kusimamia taaluma kwa bidii, akisema matokeo mazuri ya Kiru Sekondari ni kielelezo cha uongozi thabiti na ushirikiano mzuri kati ya shule, wazazi na jamii.
Niwatie moyo wazazi wote muendelee kuhimiza watoto wenu kupenda shule, kuheshimu walimu na kujituma. Mafanikio ya shule hii ni ya jamii nzima,” alisema Sanka.
Mahafali hayo yehudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na viongozi mbalimbali wa kata na wilaya, huku wahitimu wakiahidi kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri katika hatua za elimu zijazo.
Mgombea Udiwani Kata Kiru mkoani Manyara ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari ya Kiru, Joseph Siima Sanka akihutubia kwenye mahafali hayo.
0 Comments