Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki kuimba Wimbo wa Taifa wakati wa kuhitimishwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Sokoine
Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.
.............................
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema falsafa ya Mwenge wa Uhuru imekuwa dira inayoendeleza dhamira ya kuhamasisha uzalendo na ujasiri wa kupambana na maovu katika jamii na kuleta amani, upendo, maendeleo na mshikamano katika Taifa la Tanzania na Mataifa mengine.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia katika Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025 zilizofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. Amesema kupitia falsafa hiyo, nchi imefanikiwa katika mambo mengi ikiwemo kuondoa ubaguzi, ukabila, na kujenga umoja wa kitaifa, kuimarisha utawala bora, kupinga dhuluma, dharau, chuki na kupambana na ufisadi na rushwa.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Mwenge wa uhuru ulipoasisiwa ulilenga kuidhihirishia dunia na kuonesha mfano kwa Mataifa yaliyokuwa bado chini ya udhalimu wa kikoloni, maana ya Taifa huru na uwezo wa kujitawala pasipo kuingiliwa na mtu mtu yeyote.
Makamu
wa Rais ametoa wito kwa Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura, kushiriki
katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea ili kusikiliza sera za vyama
mbalimbali, na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi
watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama ambavyo Mbio
za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 zilivyobeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi
kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.
Katika
kumbukizi ya Miaka 26 tangu kifo cha Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage
Nyerere, Makamu wa Rais amesema ili kuendelea kuenzi maisha na mchango mkubwa
wa Baba wa Taifa, Watanzania wote ni vema kusimamia misingi mikuu aliyotuachia
Mwl. Julius Nyerere.
Ametaja
misingi hiyo ikiwemo kulinda uhuru wa Taifa pamoja na kudumisha umoja na amani
na kusimamia haki miongoni mwa jamii, kujenga na kuimarisha maadili mema katika
jamii hususan miongoni mwa vijana ambao ndiyo Taifa la sasa na la kesho. Pia ameongeza kwamba misingi mingine ya kusimamia ni
pamoja na kuwajibika kwa kila mwananchi
kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha na kuinua vipato na hivyo kuchangia
katika ujenzi wa Taifa pamoja na uhifadhi na utunzaji wa mazingira,
hususan kulinda vyanzo vya maji, upandaji wa miti na kufanya usafi wa
mazingira, mambo ambayo Baba wa Taifa alikuwa mfano bora wa kuigwa.
Akihitimisha
Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka 2025, Makamu wa Rais ametoa rai kwa vijana, kuendelea kutumia ubunifu, maarifa na
nguvu zao vizuri zaidi na Serikali inawaamini na itawaunga mkono. Amesema
Serikali imeendelea kuwekeza kwenye elimu, ujuzi, teknolojia, ubunifu, michezo
na utamaduni ili kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika shughuli za
kiuchumi na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza. Aidha, Ilani ya
Uchaguzi ya CCM (2025 – 2030) imeweka lengo la kuanzisha vituo vya uwezeshaji
vijana kiuchumi katika mikoa, pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana zipatazo
milioni 8.5 ifikapo 2030.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu
ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea
kuyatenda maono ya Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo, kwa kuimarisha uchumi wa Taifa, kukuza
heshima ya Tanzania kimataifa, na kulinda amani na umoja wa Watanzania.
Ameongeza
kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuenzi urithi wa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere wa uadilifu, uwajibikaji na uongozi wa kujituma kwa ajili ya watu,
kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi.
Awali
akisoma risala ya kuhitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025, Kiongozi
wa mbio hizo Ismail Ali Ussi amesema wananchi wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mitambo ya
kuchimbia visima ambayo imesaidia katika upatikanaji wa huduma za maji safi na
salama.
Pia
amesema wananchi wamemshukuru Rais kwa ongezeko la mshahara ambalo limeboresha
ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ari ya ufanyaji kazi kwa watumishi wa umma
nchini iliyopelekea wananchi kupata huduma bora.
Amesema Mwenge wa Uhuru 2025 umekagua miradi ya vijana walionufanika na mikopo ya asilimia kumi ambapo wameshukuru kwa kurejesha mikopo hiyo ambayo imesaidia kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara. Aidha amesema Vijana wamemshukuru Rais kwa kuanzisha shule za amali hapa nchini na kujenga uendelezaji Vyuo vya Veta nchini. Amesema uanzishaji wa Vyuo na Shule utasaidia vijana kupata ujuzi mbalimbali na kujiajiri kupitia juzi mbalimbali ikiwemo kutumia sayansi na teknolojia katika kutafuta utengenezaji wa bidhaa na kutafuta masoko ya bidhaa na malighafi.
Katika
Maadhimisho hayo, Kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kimezinduliwa
ambapo kimelenga kuhifadhi kumbukumbu muhimu za Kihistoria, hususan chimbuko,
maendeleo na mchango wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga mshikamano wa
kitaifa, uzalendo na kuhamasisha maendeleo. Kitabu hicho pia kinaelezea umuhimu
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kama alama ya mshikamano wa Watanzania wote bila
kujali tofauti za dini, kabila au itikadi.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Viongozi mbalimbali wakati alipowasili katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya kushiriki Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025. Tarehe 14 Oktoba 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 Bw. Ismail Ali Ussi mara baada ya kuhitimishwa kwa mbio hizo katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru wakati wa hafla ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025, iliyofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na wakimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 mara baada ya kukamilika kwa hafla ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025 zilizofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na wakimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 mara baada ya kukamilika kwa hafla ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025 zilizofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mara baada ya kukamilika kwa hafla ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Kumbukizi ya Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa kwa Mwaka 2025 zilizofanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.
0 Comments