........................................
Na Mwandishi Wetu, Manyara
Jeshi la Polisi mkoa wa Manyara limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika mkoa huo ni shwari na maandalizi yote ya kuhakikisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 yamekamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 20, 2025 amesema Jeshi hilo linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na wananchi, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu bila hofu yoyote.
Akizungumza ofisini kwake Oktoba 19, 2025, SACP Makarani amewataka wananchi waendelee kudumisha amani na kuunga mkono juhudi za vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema kuhusu watu au matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Tunawaomba wananchi wote wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura bila hofu, kwani Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake wa kikatiba kwa amani na usalama,” amesema Makarani.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua watuhumiwa wa matukio ya uhalifu, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
SACP Makarani ameongeza kuwa Jeshi hilo linaendelea na operesheni maalum za kubaini na kuwakamata wahalifu, huku likitoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na uhalifu kuacha mara moja kabla hawajakumbwa na mkono wa sheria.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayehatarisha amani na usalama wakati wa kipindi cha uchaguzi, akiwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura.




0 Comments