Subscribe Us

UMMY AOMBA KURA ZA RAIS, MBUNGE NA MADIWANI BABATI VIJIJINI

 



Mbunge Mteule wa Viti Maalum kupitia kundi la watu wenye ulemavu ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, amewataka wananchi wa Jimbo la Babati Vijijini kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Mgombea Urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mgombea Ubunge Daniel Sillo na madiwani wote wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni humo, Ummy amesema Dkt. Samia amefanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, barabara na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hivyo anastahili kupewa kura za kishindo ili aendelee na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mwenye dira na moyo wa upendo, ameleta mageuzi makubwa katika kila sekta. Ni jukumu letu kumpa kura nyingi ili aendelee kuijenga Tanzania yetu,” alisema Ummy.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Babati Vijijini Daniel Sillo, amewahakikishia wananchi ushindi mkubwa wa CCM kutokana na imani kubwa waliyonayo kwa chama hicho na kazi zilizofanywa na serikali.

“Tunakwenda kushinda kwa kishindo. Wananchi wameona kazi, wameguswa na maendeleo, na wanajua CCM ndiyo chaguo sahihi,” alisema Sillo.

Shughuli hiyo ilipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa vikundi vya ngoma za asili, muziki na vikundi vya vijana, vilivyowasha moto wa kampeni kwa hamasa kubwa.

Post a Comment

0 Comments