Subscribe Us

MBUNGE WA BABATI MJINI ASHIRIKI MSIBA WA MWALIMU MZEE MASANI QABAY, ASISITIZA AMANI

Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara Mhe.Emmanuel Khambay ( mwenye suti nyeusi) akishiriki na wananchi kwenye msiba wa Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Kata ya Singe Mzee Masani Siima Qabay.

..................................

Na Dotto Mwaibale

 MBUNGE wa Jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara Mhe.Emmanuel Khambay amewataka wananchi wa jimbo hilo na Mkoa wa Manyara kwa ujuma kuendelea kuitunza amani ya nchi na kueleza kuwa bila ya kuwepo kwa amani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo ambayo itafanyika.

Khambay aliyasema hayo wakati akishiriki kwenye msiba wa Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Kata ya Singe Mzee Masani Siima Qabay aliyefariki usiku wa kuamkia leo.

Akimuelezea Mzee Masani alisema alikuwa mtu wa aina ya kipekee kwani alikuwa akiwasaidia walimu wa shule za jirani na wanafunzi katika masuala mbalimbali ya kielimu kama vitabu na kuwaelekeza pale walipokuwa wakikwama katika ufundishaji wao  jambo ambalo atakumbukwa na wengi.

"Mzee Masani alikuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani alikuwa akisaidia walimu na wanafunzi kupata notisi mbalimbali za kujifunzia," alisema Khambay.

Aidha, Khambay aliwaomba wananchi na wazee wa jimbo hilo wampokee na kumpa ushirikiano kutokana na kuwa mgeni katika nafasi yake ya ubunge.

Mwanafunzi wa mwalimu huyo, Mwalimu Will Helmon Wilbroad Mayo alisema wataendelea kumkumbuka mwalimu huyo kutokana na upendo wake na jinsi alivyokuwa akiwafundisha kwa kujituma.

" Mzee Masani katika ukanda wetu huu hakika ameacha alama ya utumishi bora  uliotukuka kwani hakuchoka alikuwa rafiki wa watu wote," alisema Mayo. 

Katika kuhani msiba huo Mhe. Khambay aliongozana na Mbunge Mstaafu wa jimbo hilo Mzee Omary Kwaagw.

Mazishi ya Mwalimu.Masani yamefanyika leo Novemba 22,2025 Kata ya Singe.

Waombolezaji wakiwa kwenye msiba huo. Wa pili kushoto mbele ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Emmanuel Khambay.
 

Post a Comment

0 Comments