Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Tawi la Kawe la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) limepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa kwa kuwahudumia wagonjwa 8,050 ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na makazi yao huku wakipunguziwa usumbufu na gharama za usafiri kwenda makao makuu ya JKCI Upanga.
Kliniki hiyo iliyopo ndani ya jengo la Mkapa Health Plaza, Kawe, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imechangia kupunguza msongamano katika makao makuu ya JKCI na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa haraka.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja ya kliniki hiyo Mkurugenzi wa Matibabu ya Moyo JKCI, Dkt. Tatizo Waane alisema kliniki ya Kawe inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima ikiwemo wagonjwa wenye bima, wasio na bima na wale wasio na uwezo wa kugharamia matibabu.
“Wagonjwa wanaogundulika kuwa na matatizo yanayohitaji upasuaji hupelekwa katika makao makuu ya JKCI kwa hatua zaidi,” alisema Dkt. Waane.
Kwa upande wake msimamizi wa tawi hilo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Dkt. Johnstone Kayandabila alieleza kuwa kliniki hiyo pia inahudumia wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari.
“Tunahakikisha kila mgonjwa anahudumiwa ndani ya muda mfupi bila usumbufu wa foleni. Muda wa wastani wa matibabu ni saa mbili,” alisema Dkt. Kayandabila.
Nao Wagonjwa waliopatiwa huduma wameeleza kuridhishwa na ukaribu wa huduma, ufanisi na usimamizi bora unaowezesha kupatikana kwa matibabu ya mkazi haraka.
“Nimetibiwa hapa baada ya kusikia tangazo redioni. Huduma ni bora, hakuna foleni na hali yangu ya shinikizo la damu imeimarika,” alisema Khadija Ally mkazi wa Mbagala.
Mohamed Baajun mkazi wa Mabibo aliongeza, “Tunashukuru kuona JKCI inasogea karibu nasi. Inatusaidia kupunguza gharama na kupata huduma bora bila usumbufu”.



0 Comments