NA DENIS MLOWE, IRINGA
Tamasha la Lusinga Day linalofanyika kila mwaka mwezi Desemba mwishoni katika Kijiji cha Lusinga, Kata ya Dabaga, Wilaya ya Kilolo, likiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuchochea juhudi za maendeleo wamekubaliana kuanza ujenzi na ukarabati wa Shule ya Msingi Lusinga, ambayo ni miongoni mwa shule kongwe katika eneo hilo.
Akizungumza katika tamasha hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lusinga, Jakobo Mbwelwa, amewataka wananchi wa kijiji hicho waliopo ndani na nje ya kijiji kuendelea kushikamana kwa ajili ya maendeleo.
Amewahimiza wale wanaoishi nje kujiunga na kundi la Wanalusinga wanaoishi nje ili kuunganisha nguvu katika kuboresha huduma na miundombinu ya kijiji, ikiwemo shule hiyo ya msingi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji, Amasha Kisoma, amesema majengo ya Shule ya Msingi Lusinga yamechakaa na hayakidhi mahitaji ya sasa ya elimu. Amesema walimu na wazazi walishafanya kikao na kukubaliana kuanza kuchangia kwa pamoja ili kufanikisha ukarabati huo muhimu.
Kundi la Wanalusinga wanaoishi nje ya kijiji, lililoanzishwa mwaka 2019, limeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika mchango wa maendeleo ya jamii.
Kundi hilo limekuwa likitoa mahitaji kwa wazee, kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu na kutoa zawadi kwa walimu wastaafu, kama ishara ya kutambua mchango wao katika sekta ya elimu.
Katika tamasha la mwaka huu, kundi hilo limeungana na wananchi kwa kula chakula cha pamoja na kisha kukabidhi kompyuta na mashine ya kuchapisha (printer) kwa Shule ya Msingi Lusinga, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu. Pia limetoa mahitaji mbalimbali kwa watoto na wazee wenye uhitaji.
Akizungumza kwa niaba ya kundi hilo, Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dkt. Greyson Nyamoga, amesema shule hiyo imechakaa sana, hali inayohatarisha ubora wa ujifunzaji na ufaulu wa wanafunzi. Ameeleza kuwa mchango ulioanza kutolewa leo ni mbegu ya mpango mpana wa ukarabati na ujenzi wa majengo mapya ya shule.
Naye Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Lusinga, Mwalimu Athuman Hassan, amesema mazingira ya majengo ya shule hiyo si rafiki kwa elimu, hivyo ametoa rai kwa wazazi na jamii kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa mpango wa ujenzi. Ameishukuru kamati ya Lusinga Day kwa kuanzisha mchakato huo muhimu kwa shule yenye jumla ya wanafunzi 304.
Tamasha la Lusinga Day limehitimishwa kwa vifijo na matumaini mapya ya kuhakikisha Shule ya Msingi Lusinga inapata sura mpya na kuwa na mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.




0 Comments