Na Mwandishi Maalum - Arusha
Wanamichezo 450 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika walioshiriki mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yaliyofanyika jijini Arusha wamefanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo, hatua inayolenga kuimarisha usalama na ustawi wa wanamichezo chipukizi.
Zoezi hilo lilifanyika hivi karibuni katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT), ambapo wataalamu wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group waliwahudumia wanamichezo hao kwa kufanya vipimo mbalimbali vya moyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo Daktari bingwa wa bagonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema matokeo ya awali yalionyesha hali nzuri ya afya ya moyo kwa wanamichezo wengi, hali iliyowawezesha kuendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mashindano bila kikwazo.
Alisema wanamichezo hao walifanyiwa vipimo muhimu ikiwemo kipimo cha kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (ECG) pamoja na kipimo cha kutathmini muundo na utendaji wa moyo (ECHO), vipimo vinavyosaidia kugundua mapema changamoto za kiafya.
“Vipimo vya awali vilionesha kuwa wanamichezo wengi wako salama kiafya, hivyo tuliwaruhusu kuendelea na michezo. Hata hivyo, wachache tulibaini kuwa na changamoto zilizohitaji uchunguzi wa kina zaidi,” alisema Dkt. Eva.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanamichezo waliripoti dalili kama maumivu ya kifua na kizunguzungu wakati wa mazoezi hali iliyowalazimu kufanyiwa vipimo zaidi na kushauriwa kufika JKCI kwa uchunguzi wa kina ikiwemo kipimo cha Stress ECG.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Future Stars Academy, Alfred Itaeli aliipongeza JKCI kwa mchango wake mkubwa katika kulinda afya za wanamichezo, akisema huduma hiyo imewasaidia vijana kutambua mapema hali zao za kiafya na kuzuia madhara makubwa ya baadaye.
“Hii ni fursa muhimu kwa vijana kutambua afya zao mapema. Kuingiza huduma za Sports Medicine kuanzia ngazi za chini ni hatua kubwa katika maendeleo ya michezo nchini,” alisema Itaeli.
Wanamichezo walioshiriki mashindano hayo nao wameeleza kuridhishwa na huduma ya uchunguzi wa moyo, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa afya katika taaluma ya michezo.
Mchezaji wa Dream Catchers Academy kutoka Zimbabwe, Beloved Rusakaniko alisema kupima afya ya moyo kumempa uhakika wa kuendelea na michezo kwa kujiamini zaidi.
Nimefurahi sana kupima moyo wangu na kupata majibu kuwa uko salama. Kwa wanamichezo, afya ya moyo ni msingi wa mafanikio,” alisema Rusakaniko.
Naye mchezaji wa Arusha Youth Development Organization Academy, Aisha Ramadhan, alisema afya ndiyo mtaji mkubwa kwa mchezaji yeyote.
Ni mara yangu ya kwanza kupima moyo na nimejifunza kuwa bila afya huwezi kufikia malengo yako kama mchezaji,” alisema Aisha.
Mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yalifanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 15 hadi 21 Desemba 2025 katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) jijini Arusha.







0 Comments