Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo (kushoto), akisalimiana na Askofu Elisante Naman wa Kanisa la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC) wakati wa ibada ya shukrani iliyofanyika Januari 17, 2026 mkoani Manyara.
.....................................
Na Dotto Mwaibale
VITABU vitakatifu vya dini vinaeleza kuwa kauli njema zinawaongoza watu wanaomtambua Mungu kwenda Peponi na kauli mbaya huwaongoza watu wasiyo mtambua kwenda motoni.
Katika dunia ya maendeleo mbalimbali ya kijamii kauli njema zimekuwa zikihamasisha wananchi kushiriki masuala mbalimbali ya kijamii.
Kauli njema na nzuri zimekuwa na faida nyingi
katika jamii na baadhi ya viongozi wamekuwa wakizitumia ili kuwahamasisha
wananchi kushiriki shughuli za maendeleo.
Januari
17, 2026 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa
Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo alikuwa mgeni rasmi kwenye ibada maalum
ya shukrani.
Akiwa
katika ibada hiyo ya shukrani baada ya kukamilika ujenzi wa shule mpya shikizi
ya Ayaaben iliyopo Kata ya Qameyu, Kijiji cha Endaw, pamoja na uzinduzi wa
shule mpya ya msingi Mhe. Sillo alisema maendeleo yoyote hayana chama, dini wala kabila,
ndio maana Serikali inaendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo sehemu
mbalimbali za nchi bila kubagua.
Kauli
hiyo ya Mhe. Sillo ni kauli njema iliyojaa uzalendo na isiyo ya ubaguzi, ambayo kwa mpenda maendeleo yeyote
bila ya kujali dini, kabila wala chama atahamasika kushiriki shughuli za
maendeleo.
Kama
vitabu vya dini vinavyohimiza kuwa na kauli njema ndivyo inavyopaswa kuigwa na
viongozi wengine kuitumia ili kuwahamasisha na kuwaweka pamoja wananchi kushiriki
shughuli za maendeleo.
Kwenye ibada hiyo iliongozwa na Askofu Elisante Naman wa Kanisa
la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC), Mhe. Sillo alisema kuwa dhamira ya
Serikali ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata haki yake ya msingi ya
elimu, bila kujali anapotoka au anapoishi, akisisitiza kuwa miradi ya maendeleo
inalenga kuleta usawa na kuboresha maisha ya wananchi wote.
Shule hiyo imejengwa kwa juhudi za wananchi wa
kijiji hicho kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo,
ikiwa na miundombinu inayojumuisha madarasa mawili, ofisi moja pamoja na vyoo
vya wanafunzi.
Lengo kuu la ujenzi wa shule hiyo ni
kuwapunguzia usumbufu waliokuwa wakiupata wanafunzi wa wakutembea umbali mrefu
kufuata elimu katika Shule ya Msingi Endaw ambayo ndiyo shule mama.
Mhe. Sillo ametumia nafasi hiyo kuwapongeza
wananchi kwa mshikamano na moyo wa kujitolea waliouonesha katika kuchangia
ujenzi wa shule hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali
ndio msingi wa maendeleo ya kweli.
“Maendeleo hayana chama. pale wananchi
wanapoungana na Serikali, matokeo yake ni mazuri kama haya tunayoyaona leo. Hii
ni hatua kubwa kwa mustakabali wa elimu ya watoto wetu,” alisema Sillo.
Ujenzi wa shule hiyo umegharimu jumla ya Sh.
Milioni 66, ambapo wananchi wamechangia Sh. Milioni 37.5, Serikali Kuu imetoa
Sh.Milioni 25, Mfuko wa Jimbo Sh.Milioni 3, na wadau wa maendeleo wakichangia
jumla ya Sh. 480,000.
Aidha, Mhe. Sillo ameahidi kuiletea shule hiyo
vifaa vya michezo kwa ajili ya mazoezi na kuendeleza vipaji vya wanafunzi,
pamoja na kununua madawati yenye thamani ya Sh. 900,000 ili kuboresha mazingira
ya kujifunzia na
Askofu
Elisante Naman wa Kanisa la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC), ambaye
aliongoza ibada hiyo Waumini na wananchi wa Kijiji cha Endaw walimshukuru Mungu
kwa hatua hiyo kubwa ya maendeleo katika sekta ya elimu.
Aidha, katika ibada hiyo waliombea Taifa la
Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
aendelee kuiongoza nchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Qameyu
amemshukuru Mhe. Sillo kwa ushirikiano wake na mchango mkubwa katika kusimamia
na kuunga mkono miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu, akisema
shule hiyo mpya shikizi ya Ayaaben itakuwa mkombozi kwa watoto wa eneo hilo.
Shule mpya shikizi ya Ayaaben, ambayo shule
mama yake ni Shule ya Msingi Endaw, inatarajiwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa
elimu na kuongeza ari ya kusoma kutokana na ukaribu wake na makazi ya wananchi.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo (katikati), akiwa katika ibada hiyo
Askofu Elisante Naman wa Kanisa la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC) , akiongoza maombi ya kuliombea Taifa na viongozi wake.

Wananchi na Waumini wa kanisa hilo wa Kijiji cha Endaw wakiwa kwenye ibada hiyo.




0 Comments