Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) imetoa wito kwa taasisi na kampuni binafsi nchini kushiriki kuchangia huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto hususan wale wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama kubwa za matibabu.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa HTAF, Dkt. Nazihijwa Majani wakati wa ziara ya viongozi wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Geita Gold Mine (GGML) walipotembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zInazotolewa.
“Tuna malengo ya kuwafikia watoto 420 mwaka huu wanaohitaji upasuaji wa moyo. Tunaendelea kutoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia, kwani bado tunakabiliwa na changamoto ya uhaba wa malazi kwa watoto na wazazi wanaosubiri kupata huduma,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI, Dkt. Angela Muhozya alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Nyumba ya Matumaini kwaajili ya watoto wanaotoka mikoani kupata huduma za matibabu.
“Watoto na wazazi wanaotoka mbali na Dar es Salaam hukosa sehemu ya kukaa wakati wanasubiri kupata matibabu. Tunapopata msaada wa kimatibabu na miundombinu ya malazi tunagusa moja kwa moja maisha ya watoto wetu wa baadaye,” alisema Dkt. Angela.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGML), Simon Shayo alisema GGM itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha afya za watoto kupitia shughuli zake za uwajibikaji kwa jamii.
“Tunapenda kuona watoto wanakua wakiwa na afya njema. Tunaamini kuwekeza kwenye afya ni kuwekeza kwenye maisha na tutaendelea kushirikiana na JKCI kufanikisha azma hiyo,” alisema Shayo.
Wazazi wa watoto waliopatiwa huduma hiyo walitoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, JKCI, HTAF na GGM kwa msaada uliowezesha watoto wao kupata matibabu ya kibingwa na kurejea katika hali nzuri ya afya.
“Nimehangaika muda mrefu kutafuta huduma za matibabu kwa mtoto wangu kwani alikuwa na shida ya kupumua na kushindwa kucheza vizuri na wenzake, lakini kupitia msaada huu mtoto wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo na sasa anaendelea vizuri,” alisema Mariamu Rashidi kutoka Kondoa.
“Sijalipa hata senti moja kwa upasuaji wa moyo aliofanyiwa mwanangu ambao gharama yake ilikuwa ni shilingi milioni sita la laki tano. Namshukuru Mungu, Serikali, JKCI na GGML kwa msaada huu mkubwa. Naomba Watanzania wengine wajitokeze kusaidia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kama mtoto wangu,” alisema Neema Wiliam.





0 Comments