MAKAMO wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdullah akihutubia hadhara kwenye sherehe za Maulid Mkoa wa Tanga zilizofanyika Wilaya ya Pangani Februari 4, 2026.
................................
Na Dotto Mwaibale, Tanga
MAKAMO wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdullah ameongoza sherehe za Maulid Mkoa wa Tanga na kueleza kuwa maendeleo yanayofanywa na Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar yataendelea kudumu hata baada ya viongozi waliopo madarakani pindi watakapo maliza muda wao wa uongozi
Mhe. Abudullah aliyasema hayo Februari 4, 2026 wakati akihutubia kwenye hadhara ya sherehe za Maulid ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) zilizoandaliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa, Ustadhi Rajabu Abdulrahman yaliyofanyika wilayani Pangani.
Akihubia maelfu ya watu kwenye sherehe hizo Makamo huyo wa pili wa Rais Zanziba Hemed Suleiman Abdullah alisema maendeleo yanayofanywa na Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar yataendelea kuwepo hata baada ya viongozi waliopo madarakani watakapo maliza muda wao wa uongozi.
Makamo huyo wa Pili wa Rais Serikali ya Zanzibar aliwaomba wananchi kuendelea kudumisha amani pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na viongozi wote wa Taifa la Tanzania kuanzia wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya bila kusahau kuiombea nchi yetu.
"Mkoa huu, ni mwaka wa sita sasa nimekuwa mlezi wa Chama, tumeona mafanikio makubwa na ninaamini mambo yanayofanywa mnayaona kwenye maeneo yenu, niwaombe sana,tumuunge mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Na tumuunge mkono Rais Dk. Hussein Ali Mwingi, lakini pia tusimamie maendeleo yetu watu wa Tanga na nikisema hivi namaanisha, sisi wote ni wamoja na tutabaki kuwa hivyo" alisema .
"Haya maendeleo yanayofanywa yalikuwepo, kuna waliofanya sehemu zao wakapita, hata Dkt. Samia nayeye atafanya sehemu yake ataondoka, na sisi Bado tunahitajiaendeleo zaidi" alisisitiza.
Lakini pia Makamo huyo wa Rais Zanzibar aliwaomba wananchi wilayani humo kumpa ushirikiano Mwenyekiti wa CCM mkoani humo katika mambo mbalimbali anayofanya, yawe ya maendeleo pamoja nay a kiimani kama alivyoandaa sherehe za Maulid.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abdulrahman alisema Mkoa wa Tanga una amani na watu wake wanaitunza amani na katika kila jambo wapo na Rais Dk. Samia.
"Lakini pia tunaelekeza shukrani zetu kwa Rais wa Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Alli Mwinyi kwa kukubali kukuruhusu uje kujumuika na Wana Pangani katika kusherehekea nasi siku hii ya kumuenzi Mtume wetu Muhammad (SAW)," alisema Abdulrahman.
Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani Mhe. Jumaa Aweso alisema maendeleo yaliyofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia katika Wilaya ya Pangani ni makubwa hasa ujenzi wa barabara ya Tanga - Pangani ambayo ndiyo ilikuwa na changamoto kubwa.
Aweso alitaaja kero nyingine iliyokuwepo kwa mrefu wilayani humo ilikuwa ni Stendi lakini IMEKWISHA tatuliwa na Serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji utakaohudumia Wilaya za Pangani, Muheza, Korogwe na Handeni.
Aidha, Aweso aliiomba Serikali kufungua njia kutoka Bara kwenda Visiwani ambayo itapitia Wilaya ya Pangani ili kufungua fursa za biashara na uchumi kwa kupeleka maendeleo kama itakavyokuwa kwa barabara ya Tanga - Pangani, Saadani hadi Dar es salaam.
"Ombi langu kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kati Zanzibar na Pangani, kuwepo na Fast Boat, kwa maana ya kwamba watu kutoka Tanga, Mombasa, Arusha na hata wilaya za jirani wawe wanapandia hapa kwenda Zanzibar, tunaweza kufungua fursa katika Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumlawake" alisema Aweso.
Kuhusu Maulid ni Sikuu kuu ya dini ya Uislamu ya kuadhimisha kuzaliwa kwake Mtume Muhammad takriban mwaka 570 BK.
Sikukuu au sherehe hiyo inafuata kalenda ya Kiislamu ambapo Waislamu wa dhehebu la Sunni husheherekea Tarehe 12 Rabi’-Ul- Awwal kwa mujibu ya kalenda ya Kiislamu ya Alhijria huku Waislamu wa dhehebu la Shia husheherekea Tarehe 17 Rabi'-ul-Awwal.
Wataalamu wa historia wengine wanasema ya kwamba sherehe ya Maulid imeanzishwa mnamo karne ya 12 BK.
Kuna Waislamu kadhaa wanaokataa sherehe hiyo kwa sababu hakuna Sunna wala hadithi ya Muhammad mwenyewe kuhusu kusheherekea ya maulid yake. Lakini kwa ujumla ni sikukuu inayopendwa sana na Waislamu wengi duniani.
Misri Maulid ni kati ya sikukuu za Kiislamu zinazokumbukwa sana na Waislamu.
Katika Afrika Mashariki sherehe ya maulid huko Lamu Mombasa nchini Kenya imejulikana hasa ikivuta wageni kutoka pande zote za Afrika ya Mashariki hadi Uarabuni.
Katika sherehe za Mulid zinaambatana na mikutano pamoja na kusikia mashairi juu ya maisha ya Mtume na mambo mengine mengi ya kumtukuza Mwenyezi Mungu.
Sharifu Ahmad Badawy anasema kuwa sehemu inapofanyika sherehe za Maulid tukio kubwa huwa ni kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W) ambapo Allah huwapa thawabu waandaaji wa Maulid pamoja na wale ambao wanafuata kula pirau.
Kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni jambo kubwa kiimani na kuandaa Maulidi kila mtu anaweza kuandaa kutokana na jinsi alivyojiandaa kiimani kumswalia Mtume Mohammad (S.A.W), ambaye anawakufungulia neema kubwa katika maisha.
Hapa napenda kumzungumzia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abdulrahman kwa jinsi anavyo andaa Maulid kila mwaka na kuhudhuriwa na maelfu ya waislamu na wasiyo waislamu ili ni jambo kubwa la kiimani tunamuombea Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema na kumuongezea neema kwa kuandaa Maud kila mwaka.



0 Comments