Subscribe Us

BABATI DC WATIKISA SHEREHE ZA WANAWAKE DUNIANI

Na John Walter-Babati

Jamii imetakiwa kushirikiana kikamilifu katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ikiwemo Jeshi la Polisi na viongozi katika ngazi mbalimbali badala ya kukaa kimya.

Wito huo umetolewa na OCD wa Wilaya ya Babati Ernesta Mwambinga katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Halmashauri ya Wilaya ya Babati akiwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo.

Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vina madhara makubwa kwa jamii ikiwemo kuathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kusimama na kupinga vitendo hivyo.

Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Babati chini ya Mkurugenzi Mtendaji Anna Mbogo kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo isiyo na riba inayosaidia kuinua wanawake kiuchumi.

Maadhimisho hayo yamefanyika machi 6,2026 katika Shule ya Msingi Vilima Vitatu, Kata ya Nkaiti yakiongozwa na kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira 2050.”

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Maendeleo Mwandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Dickson Matei amesema tangu serikali ifanye maboresho ya mpango wa mikopo isiyo na riba mwaka 2024, halmashauri hiyo imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Ameongeza kuwa kuanzia Januari hadi Machi 2026, halmashauri hiyo imetoa zaidi ya shilingi milioni 200 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, huku hundi ya mikopo hiyo ikikabidhiwa leo kwa vikundi 33.

Katika kuadhimisha siku hiyo, shughuli mbalimbali za kijamii zilifanyika ikiwemo upandaji wa miti pamoja na ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Burunge.

Post a Comment

0 Comments