Subscribe Us

MGONJWA ALIYEDAIWA KUZUILIWA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA AFARIKI DUNIA OCEAN ROAD



Celina John Furaha akiwa amekaa eneo la wageni Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es  Salaam huku amepigwa butwaa kufuatia kifo cha mpendwa dada yake Ester aliyekuwa akimsaidia wakati wa kuumwa kwake.

............................

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

MGONJWA Ester John Furaha (32) ambaye alipewa rufaa kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu baada ya kudaiwa kuzuiliwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa  deni la Sh.1,175,000 amefariki dunia katika taasisi hiyo.

Ester ambaye alikuwa akipatiwa matibabu ghorofa namba tatu wodi namba 303 amefariki dunia Machi 21, 2026 majira ya saa 8 mchana wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Taasisi  ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Mark Mseti alipopigiwa simu alishukuru kupata taarifa hiyo na kueleza kuwa kwa kuwa hayupo kazini ataulizia idara ya mapokezi ili kujua mgonjwa huyo alipokelewa na kusajiliwa lini, na alikuwa amelazwa wodi namba ngapi na lini alifariki.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mdogo wa marehemu aliyekuwa akimuuguza, Celina Furaha alisema wakiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa Machi 20,2026 majira ya saa 4 asubuhi  waliruhusiwa  kuondoka.

“Tuliondoka saa 9 jioni na gari la wagonjwa huku mgonjwa akiwa ametundikiwa dripu  na kueleza kuwa walifika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road saa 5, usiku ambapo walipokelewa chumba cha wagonjwa wa dharura na kupatiwa huduma ya awali kwa kumtundikia dripu nyingine tena kabla ya kupelekwa wodini,” alisema Celina.

“Wauguzi wa taasisi hiyo na wafamasia walijitahidi sana kumuhudumia mgonjwa hata baadhi ya dawa ambazo zilikuwa zikihitajika walimpa na mimi nililipia Sh. 30,000 kwa dawa za awali zilizokuwa zikihitaji lani ndiyo hivyo haikuwa riziki yetu jana (Machi 21, 2026) majira ya saa 8 mchana alifariki,” alisema Celina.

Aidha, Celina alisema taarifa ya kufariki kwa dada yake zimewafikia ndugu zao, lakini changamoto kubwa inayowakali ni namna ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani kwao Kata ya Wareta wilayani  Hanang’  mkoani Manyara kwa ajili ya taratibu za maziko.

Kaka wa marehemu aitwaye Paulo Nyangqura alisema taarifa hiyo wameipokea kwa masikitiko makubwa ila changamoto waliyonayo ni ya kiuchumi.

Hata hivyo, alisema wanatarajia kufanya kikao baina ya ndugu za mama yake marehemu na mume wake kuona jinsi ya kufanya.

“Kama mwili utafanikiwa kufika maziko yake yatafanyika Kijiji cha Bashanga Kata ya Wareta Katesh  Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara,” alisema Nyangqura.

 Grace Nicholaus ambaye amelazwa kwa muda mrefu Taasisi ya Saratani Ocean Road aliyekuwa akimsaidia kumuelekeza Celina kumuuguza dada yake amewapongeza madaktari, wafamasia na wauguzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa jitihada kubwa walizozifanya kumtibia Ester tangu alipofikishwa hospitalini hapo.

“Kwa kweli jitihada kubwa imefanyika kumtibia Ester ingawa alikuwa amechoka sana lakini yote tunamuachia Mungu ambaye amempenda zaidi,  kikubwa ni kumuombea akapumzike kwa amani,” alisema Nicholaus.

Pamoja na madhira mbalimbali aliyoyapitia Ester,  amekwisha fariki kinachohitajika hivi sasa ni kusafirisha mwili wake kwenda nyumbani kwao Kijiji cha Bashanga kwa maziko , ndugu zake wamedai hawana uwezo wa kusafirisha mwili wake,  hivyo kupitia habari hii Watanzania kwa ujumla wetu tunaombwa kuisaidia familia hiyo katika jambo hilo.

Kwa yeyote atakaye guswa kuwasaidia anaweza kuwasiliana na Grace Lucas Nicholaus ambaye yupo na mdogo wa marehemu, Celina Furaha kwa kutoa mchango kupitia namba 0683917960 na jina litakalo tokea ni Grace Lucas Nicholaus na Mungu atawabariki.

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990

Ester John Furaha enzi za uhai wake

Grace Lucas Nicholaus mgonjwa wa muda mrefu anayetibiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ambaye alikuwa akimsaidia Ester na kumuelekeza mdogo wake katika masuala mbalimbali wakati wa kumuuguza dada yake.

Muonekano wa Jengo la Utawala Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam.
 

Post a Comment

0 Comments