Subscribe Us

SAKATA LA MGONJWA ALIYEDAIWA KUZUILIWA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA LAFIKIA TAMATI

Muonekano wa Jengo la Utawala la Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma

............................... 

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

SAKATA la Mgonjwa Ester John Furaha aliyedai kuzuiliwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma kwa kushindwa kulipa gharama ya matibabu licha ya kupewa rufaa kwenda Taasisi ya Kansa ya Ocean Road jijini Dar es Salaam limefikia tamati baada ya kuruhusiwa.

Akizungumza Machi 20, 2026 na mwandishi wa habari hii, Afisa Uhusiano katika  Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Jeremia Mwakyoma alisema tayari mgonjwa huyo ameruhusiwa kwenda kuendelea na matibabu yake Taasisi ya Kansa Ocean Road Jijini Dar es Salaam.

“Kuna rufaa za aina mbili  ipo ya kawaida na nyingine anaposafirishwa inahitajika mgonjwa kuwekewa oksijeni ya kupumulia kama inavyohitajika kwa Ester lakini bila ya hivyo ataweza kupoteza maisha,” alisema Mwakyoma.

Mwakyoma alisema kwa kawaida mgonjwa akipatiwa rufaa hata kama alikuwa na deni hawezi kuzuiliwa atakwenda hospitali husika na suala la malipo ya deni lake yatafuata baadae wakati akiendelea na matibabu.

Awali mdogo wa mgonjwa huyo Celina Furaha alisema  kuwa dada yake alizuiliwa kutoka hospitali hapo mpaka alipe  deni la Sh. 1,175,000 alizokuwa akidaiwa baada ya kupatiwa matibabu na kueleza kuwa rufaa hiyo alipewa Machi 18, 2026.

“Tumeruhusiwa leo Machi 20, 2026 kuondoka kuelekea Taasisi ya Kansa ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu tunashukuru sana na Mungu hawabariki ingawa nilitamani turudi nyumbani tukatafute hela za matibabu,” alisema Celina.

Celina alisema wamekuwepo katika hospitali hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu wakitokea Hosptali ya Makiungu wilayani Ikungi mkoani Singida ambapo walibaini kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa na wamelipia matibabu yake zaidi ya Sh. Milioni 3.2 na kuishiwa fedha huku wakiishi kwa msaada wa wasamaria wema.

Mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu  wakati akihutubia katika uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kawe jijini Dar es Salaam moja ya ahadi yake ilikuwa ni kupiga marufuku kuzuia miili ya marehemu ambayo ilikuwa ikizuiliwa kwa kushindwa kuilipia katika hospitali mbalimbali nchini.

Hata hivyo katika hali ya kawaida kwa wagonjwa kama Ester inapaswa kuwekwa mwongozo wa wazi ili kuondoa hali hiyo ya kuzuiliwa kufuatia kuwa na deni badala yake wapelekwe haraka kuendelea kupatiwa matibabu jambo litakalosaidia kuokoa maisha yao kuliko  kuzuiliwa wodini kama ilivyodaiwa kufanywa kwa mgonjwa huyo.

Kwa ujumla hatua ilichukuliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kumruhusu mgonjwa huyo kwenda kuendelea kupata matibabu yake Taasisi ya Kansa ya Ocean jijini Dar es Salaam inapaswa kupongezwa.

Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.

Post a Comment

0 Comments