Subscribe Us

SILLO AHUDHURIA BARAZA LA IDDY QASH, ASISITIZA AMANI.

Na Mwandishi Wetu- Babati
--------------------------------------------

Baraza la Iddy katika Kata ya Qash, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, limewataka wananchi kuendelea kudumisha amani ili kuwezesha ibada kufanyika kwa utulivu pamoja na kukuza maendeleo ya jamii.

Akizungumza katika baraza hilo lililofanyika katika Msikiti wa Orngadida Mlimani, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Spika wa Bunge, Mheshimiwa Daniel Sillo, amesisitiza umuhimu wa amani akieleza kuwa ni msingi mkubwa wa ustawi wa taifa na maendeleo ya wananchi.

Sillo amewataka pia viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi pamoja na viongozi wake ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye mshikamano.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameongoza uchangiaji maalum kwa ajili ya ujenzi wa jiko la kupikia katika Madrasa ya Zaharau, akilenga kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na kupikia.

Amesisitiza kuwa ujenzi huo uanze mara moja kuanzia kesho, huku akitoa maelekezo ya kupatikana kwa fundi na kuandaliwa kwa bajeti ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Sillo ameahidi kusaidia upatikanaji wa mikeka ya kusalia kwa ajili ya msikiti huo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono shughuli za ibada kwa waumini.

Kwa upande wake, Katibu wa Taasisi ya Zaharau, Abdala Shaibu, amemshukuru Mbunge huyo kwa moyo wake wa kujitolea na kujali maendeleo ya taasisi hiyo.

Naye Imamu wa Msikiti wa Zaharau Orngadida Mlimani, Mussa Abdala, amempongeza Sillo kwa mchango wake, akieleza kuwa hatua hiyo italeta manufaa makubwa kwa wanafunzi na waumini kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments