Na Dotto Mwaibale, Dodoma
WABUNGE wa Mkoa wa Manyara wakiongozwa na Naibu Spika wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daniel Sillo, wananchi wa Manyara na Watanzania
kwa ujumla, mgonjwa Ester John Furaha ambaye
anapitia wakati mgumu kutokana na ugonjwa wa kansa unaomsumbua anaomba msaada
wenu.
Ester John Furaha anayesumbuliwa na kansa ya kichwa hali
yake imetetereka licha ya kupata matibabu katika hospitali mbalimbali na
anakabiliwa na madeni makubwa kutokana na fedha anazokopa kwa ajili ya
matibabu.
Mapema wiki hii (Machi 18, 2026) baada ya kupewa rufaa ya
kwenda kutibiwa Taasisi ya Kansa Ocean Road Jijini Dar es Salaam inadaiwa alizuiliwa Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini
Dodoma mpaka alipe Sh.1, 175, 000 alizokuwa akidaiwa baada ya kutibiwa.
Mgonjwa huyo Machi 20, 2026 aliruhusiwa kuondoka katika
hospitali hiyo akiwa na mdogo wake Celina anaye muuguza baada ya habari yake
kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Celina Furaha (27) alisema
wao ni wakazi wa Kijiji cha Changanyika kilichopo Katesh wilayani Hanang’ Mkoa
wa Manyara.
Celina alisema dada yake Ester mwenye watoto wanne alianza
kuumwa mwaka juzi ambapo alikuwa akitibiwa Hospitali ya Tumaini iliyopo Hanang’
mkoani humo lakini pamoja na kupata matibabu hali yake iliendelea kuwa mbaya.
Alisema mume wake alipoona ameelemewa na madeni baada ya
kukopa fedha kwa ajili ya matibabu yake alikimbia na mpaka sasa hajulikani
alipo.
“Mume wake baada ya kuona amezidiwa na madeni aliondoka bila
ya kuaga na hatujui halipo hivyo tunaangaika na mgonjwa huku tukikabiliwa na
madeni makubwa ambayo sijui tutayalipaje,” alisema Celina.
Alisema baada ya hali yake kuzidi kuendelea kuwa mbaya
alipewa rufaa ya kwenda Hospitali Teule ya Makiungu iliyopo Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida ambapo alitibiwa kwa wiki kadhaa na baada ya vipimo aligundulika
kuwa na kansa kwenye kichwa.
Aliongeza kuwa baada ya hapo alipewa rufaa ya kwenda
Hospitali ya Benjamin Mkapa lakini hata hivyo walilazimika kukaa katika hospitali
ya Makiungu mpaka walipopata fedha Sh. Milioni moja waliyokopa ambayo
iliwasaidia kuanza kupata matibabu hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Alisema tangu wawepo katika hospitali hiyo wametumia zaidi ya Sh.
Milioni 3.2 ambazo wamezikopa kwa watu mbalimbali na wanadaiwa.
Aidha, Celina alisema hawana mtu wanayemtegemea zaidi ya kilimo
cha mkono kwani baba yao alifariki na
mama yao ni mlemavu wa macho (haoni) na pia anasumbuliwa na ugonjwa wa kifafa.
“Tunapita katika wakati mgumu maisha yetu ni ya mateso tumekuwepo hapa hospitalini kwa zaidi ya miezi mitatu tukipatiwa msaada wa chakula na mambo mengine na wasamaria wema ambao wanafika kuwaona ndugu zao ambao ni wagonjwa,” alisema Celina huku akikata tamaa na kutamani warudi nyumbani kwao Katesh.
Mgonjwa Ester na mdogo wake anayemuuguza tayari wameondoka
jana Machi 20, 2026 majira ya saa 9 mchana kuelekea Taasisi ya Kansa ya Ocean
Road jijini Dar es Salaam huku wakiwa hawajui hatima yao watakapokuwepo kwenye
jiji hilo kubwa ambapo watahitaji chakula, matibabu na mambo mengine ya kibinadamu.
Kupitia habari hii Celina anawaomba wabunge wa Mkoa wa
Manyara wakiongozwa na Naibu Spika Daniel Sillo, viongozi na makundi mengine na
Watanzania kwa ujumla waweze kuwasaidia katika wakati mgumu wanaopitia ikiwa pamoja
na kulipa madeni wanayodaiwa.
Kwa mtu yeyote atakaye guswa kuwasaidia anaweza kuwasiliana
na mwandishi wa habari hii kwa namba 0754362990, Mungu atawabariki.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu
0754362990.




0 Comments