........................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAKATI Wanawake wakiwa katika madhimisho ya kusherehekea siku yao Mwalimu Helena Mahamba (42), wa Shule ya Msingi Unyakhae katika Manispaa ya Singida ambaye alitamani kushiriki na wanawake wenzake katika siku yao hiyo yupo kitandani akipambania hali mbaya ya afya kutokana na ugonjwa wa kisukari unaomsumbua kwa zaidi ya miaka 17, hali inayomlazimu kuwaomba Watanzania kujitokeza kumsaidia gharama za matibabu.
Mwalimu huyo anaishi kwa kutegemea sindano za insulin kila siku baada ya kongosho lake kushindwa kufanya kazi. Kutokana na hali hiyo, amekuwa akitumia muda mwingi akiwa amelala kitandani huku akisumbuliwa na maumivu makali ya viungo, kuvimba miguu na mwili mzima, jambo linalomfanya ashindwe hata kutembea.
“Naomba msaada wananchi wenzangu, ugonjwa wa kisukari unanisumbua sana. Imefika wakati sitoki ndani, miguu inavimba na mwili mzima. Licha ya kuwa na bima ya afya, sipati dawa zote ninazohitaji hivyo nalazimika kununua mwenyewe,” alisema Mahamba kwa huzuni.
Alieleza kuwa kuna wakati hali yake ilizidi kuwa mbaya na kulazimika kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambapo alikuwa akitakiwa kulipa Sh.100,000 kwa siku, gharama ambazo hakuweza kuzimudu. Amesema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni ukosefu wa fedha za matibabu na lishe maalum anayohitaji kama mgonjwa wa kisukari.
Mahamba, ambaye alianza kuugua mwaka 2010, amesema kwa sasa anajidunga sindano mbili za insulin kila siku, hali inayomchosha na kumfanya apoteze hamu ya kula na hata ya kuendelea na maisha ya kawaida.
“Naombeni msaada Watanzania wenzangu, nishikeni mkono kwa chochote mtakachojaliwa na Mwenyezi Mungu. Ni kweli mimi ni mwalimu, lakini imefika mahali nimeishiwa kila kitu. Ndugu zangu nao wamechoka kunisaidia kwa muda mrefu,” alisema huku akitokwa na machozi.
Mwalimu Helena Mahamba anahitaji msaada wa haraka wa fedha kwa ajili ya matibabu, ununuzi wa dawa na lishe maalum. Watanzania, taasisi za Serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na watu binafsi wanahimizwa kujitokeza kumsaidia ili kuokoa maisha yake.
Kwa yeyote atakayeguswa kumsaidia, anaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0787 820053 au 0759 521565. Pia anaweza kutuma mchango kupitia Akaunti Namba 0152364578800, Benki ya CRDB, kwa jina la Helena Nyahuru Mahamba.
Mwenyezi Mungu awabariki wote watakaoguswa kumsaidia, kwani mchango wowote, mkubwa au mdogo, utakuwa faraja na msaada mkubwa kwake katika kipindi hiki kigumu cha maisha yake.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990



0 Comments