Subscribe Us

𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐈𝐖𝐀 𝐊𝐖𝐄𝐍𝐃𝐀 𝐊𝐔𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀 𝐌𝐈𝐊𝐔𝐓𝐀𝐍𝐎 𝐍𝐀 𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐂𝐇𝐈 𝐍𝐀 𝐊𝐔𝐓𝐀𝐓𝐔𝐀 𝐂𝐇𝐀𝐍𝐆𝐀𝐌𝐎𝐓𝐎 𝐙𝐀 𝐊𝐈𝐔𝐒𝐀𝐋𝐀𝐌𝐀

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa akizungumza na kwenye hafla ya kumpongeza Koplo Stella Lyimo kwa kupata tuzo.

Baadhi ya Askari Polisi wakiwa kwenye ukumbi

Na Hellen Mtereko,Mwanza

Wakuu wa Polisi wa Wilaya, Wakuu wa vituo, Maafisa Polisi Jamii ngazi ya Mkoa, Wilaya, na Wakaguzi wa Kata wametakiwa kuacha kukaa ofisini badala yake waende kwenye maeneo ya kata kwa ajili ya kufanya mikutano na wananchi inayolenga kuzuia, kudhibiti uhalifu na kutatua changamoto mbalimbali za kiusalama katika maeneo yao ya kazi.

Rai hiyo imetolewa Jumatano ya Aprili 29, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kumpongeza Koplo Stella Lyimo ambaye ni Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana aliyepata tuzo ya mwanamke kinara katika kipengere cha Ustawi wa Jamii ambapo alitajwa kufanya vizuri katika kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii.

Mutafungwa amesema askari polisi wanawajibu wa kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi kwa kuwahudumia wananchi sanjari na kulinda raia na mali zao ili wawe na taasisi ambayo inaheshimika na kupendwa na wananchi.

“Kwa wakaguzi wa kata hamieni kwenye kata zenu mkatimize wajibu wenu wa kufanya mikutano na wananchi, zungumzeni na makundi mbalimbali ili mfahamu migogoro iliyopo ndani ya familia ili kuhakikisha mnatatua migogoro hiyo kabla haijaleta madhara”Alisema Mutafungwa.

Amesema Jeshi la polisi linadhamana kubwa ya kuhakikisha linatoa huduma kwa wananchi wakati wote, hivyo askari wote waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia kazi wanazozifanya.

“Nawahimiza watendaji wote kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia nidhamu uadilifu, uwajibikaji pamoja na haki kwa wananchi” Alisema Mutafungwa.

Aidha ameeleza kuwa matukio ya mauaji yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya mitaa wanao uwezo wa kuyazuia kwani mauaji mengine yanasabishwa na migogoro ya ardhi ya muda mrefu, imani potofu za kishirikina.

“Nendeni mkaingilie kati, kwa kuwapa elimu kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmebadilisha makundi kwenye familia na jamii hatua itakayosaidia vitendo hivyo kumalizika” Alisema Mutafungwa.

Kwa upande wake Mkaguzi Kata wa Kata ya Mabatini iliyoko Wilaya ya Nyamagana Mkoani hapa, Shabani Kashakala amesema maelekezo yaliyotolewa na kamanda Mutafungwa ameyapokea na kuahidi kuyatekeleza kikamilifu.

Kashakala ameeleza kuwa wanapokuwa karibu na jamii wanapata fursa ya kufahamu migogoro inayoendelea ikiwemo ya kifamilia, Ardhi pamoja na yawafugaji.

Post a Comment

0 Comments