Subscribe Us

POLISI BABATI WAPATIWA ELIMU MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Elimu kuhusu matumizi ya Nishati safi ya kupikia ikitolewa kwa Askari Polisi Mjini Babati mkoani Manyara.
.........................................

MAAFISA wa Jeshi la Polisi mjini Babati mkoani Manyara wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majiko ya kisasa yanayotumia umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhamasisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Elimu hiyo imetolewa  Aprili 2, 2026 katika ukumbi wa Polisi Messi uliopo Babati, ambapo Afisa Uhusiano kwa Umma wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),  Mkoa wa Manyara, Samwel Mandari, amesema matumizi ya majiko ya umeme ni nafuu, yanaokoa muda na gharama, pamoja na kuwa salama kwa mtumiaji.

Mandari ameeleza kuwa majiko hayo ya kisasa aina ya Pressure Cooker kutoka kwa wakala Sescom, aliyethibitishwa na kampuni ya Sescom, yana uwezo wa kuandaa chakula kwa muda mfupi, hivyo kusaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya nishati.

Amesisitiza kuwa maafisa hao wanapaswa kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa jamii, kwa kuwa matumizi ya nishati safi ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kulinda mazingira na kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki.

Kwa upande wake, Inspekta Sebastian Mbuwa, akizungumza kwa niaba ya askari waliopata mafunzo hayo, ameishukuru TANESCO kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu, na kuomba iendelee kutolewa mara kwa mara ili kuwajengea uelewa zaidi.

Amesema elimu hiyo itawasaidia si tu katika matumizi yao binafsi bali pia kuwa chachu ya mabadiliko kwa jamii inayowazunguka.Picha ya pamoja baada ya mafunzo


Elimu zaidi ikitolewa

Chanzo WH-NEWS
 

Post a Comment

0 Comments