Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Haron Makandi, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Adolf Mkenda wakati wa Kongamano la Kitaifa kuhusu matumizi ya QR Code na AI. Mei 20, 2026.
..................................
Na Mwandishi Wetu, Arusha
SERIKALI imejipanga kuharakisha kukamilika kwa sera ya matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) ili ianze kutumika rasmi nchini huku ikisisitiza matumizi sahihi ya teknolojia hiyo kwa kuzingatia maadili na usalama wa taarifa.
Hayo yalisemwa Mei 19, 2026 jijini Arusha na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Haron Makandi kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Adolf Mkenda wakati wa Kongamano la Kitaifa kuhusu matumizi ya QR Code na AI.
Dkt. Makandi alisema serikali inalenga kuhakikisha sera hiyo inakamilika mapema ili kusaidia kukuza matumizi ya AI, kuimarisha ubunifu pamoja na kuweka mwongozo wa matumizi ya teknolojia hiyo nchini.
Alisema kwa sasa sera hiyo ipo katika hatua ya rasimu ndani ya serikali huku maboresho mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kutumika rasmi.
“Tunataka kuwa na mfumo unaotoa mwongozo wa matumizi sahihi ya AI huku tukihakikisha maadili, usalama wa taarifa na matumizi yenye tija vinaendelea kuzingatiwa,” alisema Dkt. Makandi.
Kongamano hilo lililoandaliwa na ScanCode T Limited limewakutanisha wadau wa teknolojia, taasisi za serikali, sekta binafsi pamoja na wafanyabiashara kwa lengo la kujadili matumizi ya AI na QR Code katika kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma.
Mkurugenzi wa ScanCode T Limited, Faustine Mgimba alisema teknolojia za ScanCode zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi na wafanyabiashara katika dunia ya sasa ya kidigitali kwa kurahisisha malipo, utoaji wa taarifa na huduma mbalimbali kwa njia ya haraka na salama.
Alisema matumizi ya QR Code yanasaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu na makaratasi huku yakiongeza ufanisi katika biashara, taasisi na huduma za kijamii, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali nchini.
Naye Afisa Mafunzo wa kampuni hiyo, Abdulwahid Ali Khamis alisema teknolojia hizo zimekuja kusaidia kurahisisha utendaji kazi na kuongeza tija badala ya kuondoa ajira za watu.
Alisema dunia ya sasa inaelekea kwenye matumizi ya mifumo ya kidigitali isiyotegemea makaratasi wala fedha taslimu huku teknolojia za QR Code zikirahisisha malipo na utoaji huduma kwa njia salama na ya haraka.
Aidha, aliwataka vijana kutumia teknolojia kwa maendeleo na kujiepusha na matumizi mabaya yanayoweza kusababisha madhara kwa jamii na kwao wenyewe.
Kongamano hilo likiendeleaMada zikitolewa
Nyaraka wakikabidhiana wakati wa kongamano hilo.







0 Comments