Subscribe Us

𝐉𝐄𝐒𝐇𝐈 𝐋𝐀 𝐌𝐀𝐆𝐄𝐑𝐄𝐙𝐀 𝐋𝐀𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐇𝐈𝐌𝐈𝐒𝐇𝐎 𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐘𝐀 𝐖𝐈𝐊𝐈 𝐘𝐀 𝐔𝐓𝐔𝐌𝐈𝐒𝐇𝐈 𝐖𝐀 𝐔𝐌𝐌𝐀 𝟐𝟎𝟐𝟔

Jeshi la Magereza kwa mara nyingine tena linashiriki kikamilifu kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2026 Maadhimisho ambayo ni moja ya Maazimio ya Umoja wa Afrika (AU). 

Hivyo, Jeshi la Magereza linawakaribisha wananchi wote wa Tanzania kutembelea Banda la Magereza katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia Leo Juni 16 hadi 23, 2026.

Maonesho hayo yatawakutanisha Wananchi, Taasisi za Umma na Wadau mbalimbali kwa lengo la kuelezea Dhima, Dira, Mafanikio, Changamoto zilizopo katika suala zima la urekebishaji Wafungwa, kutoa huduma na taarifa mbalimbali muhimu kuhusu shughuli zinazotolewa na Serikali kwa Wananchi kupitia Jeshi la Magereza na kuueleza Umma juu ya Mageuzi ya kisayansi yanayofanywa sasa na Jeshi katika uendeshaji na urekebishaji Wafungwa.

Pamoja na kutoa huduma hizo, Jeshi la Magereza kupitia Maadhimisho haya linatoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa kwa wafungwa na mahabusu pamoja na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zinazofanywa Magerezani kama mbinu za urekebishaji wafungwa. Wananchi pia wanapata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata ufafanuzi wa papo kwa papo kutoka kwa Maafisa Magereza waliopo katika Banda hilo.

Sambamba na utoaji wa huduma hizo, Jeshi la Magereza linaendelea kutoa elimu kuhusu shughuli za urekebishaji wa wafungwa, ikiwemo elimu ya maadili, stadi za maisha, mafunzo ya ufundi stadi, ushauri nasaha na programu nyingine zinazolenga kuwawezesha wafungwa kubadilika na kujiandaa kurejea katika jamii wakiwa raia wema na wenye tija kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Kupitia elimu hiyo, wananchi wanahamasishwa kutambua mchango wa Programu za urekebishaji katika kupunguza uhalifu nchini, kuwajengea wafungwa uwezo wa kujitegemea na kuimarisha usalama wa jamii kwa ujumla.

Aidha, elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Magereza katika mchakato wa urekebishaji na urejeshwaji wa wafungwa katika jamii baada ya kutumikia vifungo vyao na kuondoa unyanyapaa hivyo kuwapokea na kuwashirikisha Wafungwa wanaorudi kutoka Magerezani katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi kwa Umma 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”

Post a Comment

0 Comments