Subscribe Us

TOIMA: WAFUGAJI ZAMA ZIMEBADILIKA SOMESHENI WATOTO

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara,Peter Toima (katikati), ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa kwenye mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari ya LoIborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara yaliyofanyika Oktoba 10,2025.
..........................................

Na Mwandishi Wetu, Manyara

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara,Peter Toima, amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kuwekeza zaidi katika elimu, akisisitiza kuwa katika zama za sasa, elimu ndiyo njia ya kweli ya ukombozi na maendeleo.

Amezungumza hayo katika mahafali ya 12 ya kidato cha nne yaliyofanyika Shule ya Sekondari LoIborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara Oktoba 10,2025.

“Tofauti na zamani, leo elimu ndiyo msingi wa mafanikio. Nawaomba wazazi wa jamii ya wafugaji kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati. Wape watoto wote – wa kike na wa kiume – nafasi sawa ya kupata elimu, maana zama zimebadilika,” alisemaToima.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Loiborsitet, Mwalimu Fabian Dorie, amesema shule hiyo imepiga hatua kubwa ya maendeleo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 ikiwa na wanafunzi watano pekee, hadi kufikia mwaka 2025 ikiwa na wanafunzi 388.

Mwalimu Dorie amesema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa jengo la utawala, hali inayowalazimu walimu kutumia darasa kama ofisi na maktaba. Ameziomba mamlaka husika, hususan serikali, kusaidia kujenga jengo la utawala ili kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa elimu.

Kwa upande wake, Mchungaji Patrick Kajila amewahimiza wazazi kushirikiana na walimu ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na elimu yenye tija, akisema:

“Watoto hawa ndio nguvu kazi ya taifa kesho. ushirikiano wa wazazi na walimu ni nguzo ya mafanikio ya elimu.”

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 57 walihitimu kidato cha nne katika shule hiyo iliyopo Wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.

Wahitimu wa kidato cha nne wakiwa kwenye maandamano ya ufunguzi wa mahafali hayo.
 

Post a Comment

0 Comments